Main Article Content
Uchipuzi wa kileksika katika mashairi ya Shaaban Robert
Abstract
Shaaban Robert ni miongoni mwa waandishi wenye hadhi ya juu katika fasihi ya Kiswahili kutokana na ukubwa na upevu wa mchango wake katika fasihi hiyo. Kuna tahakiki nyingi zikiwemo vitabu, tasnifu na makala ambazo zimeandikwa juu ya tungo zake. Hata hivyo, hatuwezi kusema kwamba uchunguzi juu ya kazi za kigogo huyo umetosha. Bado wahakiki wana kazi kubwa mbele yao. Shaaban Robert aliasisi na kuendeleza tanzu kama vile riwaya, wasifu, tawasifu na insha. Lakini ni katika ushairi ambapo alitoa mchango mkubwa zaidi. Tahakiki nyingi juu ya mashairi yake zinashughulikia maudhui zaidi kuliko fani. Mathalan: A. G. Gibbe (1980), E. K. Kezilahabi (1976) na F. E. M. K. Senkoro (1988). Hatusemi kwamba kuna ubaya wowote wa tahakiki kuelemea kwenye maudhui. Hata hivyo, kuna mengi sana katika fani ya mashairi ya Shaaban Robert ambayo yanastahili kushughulikiwa. Hivyo, mchango wa makala hii katika kuziba pengo hilo ni kuchunguza kipengele kimoja tu katika mtindo wa mashairi ya Shaaban Robert, yaani msamiati, na haswa jinsi mshairi anavyoepukana na ukawaida kutokana na ustadi wake wa kutumia lugha teule. Tunaitathmini leksisi hiyo kwa kuchunguza sababu za uteuzi na umuhimu wake wa kimaana. Kwa ujumla, mwelekeo wa makala ni wa elimumitindo.