Main Article Content
Udondoshaji wa Vipashio katika Vichwa vya Magazeti ya Kiswahili
Abstract
Uandishi wa magazeti umeonekana kuwa wa kipekee kwani hutumia mitindo mbalimbali ya uandishi ukiwamo udondoshaji wa vipashio. Tafiti zinaonesha kwamba, udondoshaji wa vipashio katika vichwa vya magazeti hufanyika kwa lengo maalumu. Mathalani, inaweza kuwa ni kwa lengo la uwekevu, kuleta hamasa na mguso kwa msomaji. Licha ya kudhihirika kwa mtindo huu, tafiti zilizochunguza udondoshaji katika magazeti ya Kiswahili zinataja kiambishi njeo pekee kama kipashio kinachodondoshwa katika uandishi wa vichwa vya magazeti ya Kiswahili. Aidha, tafiti tangulizi zinaonesha kuwa vipo vipashio vingine vinavyodondoshwa katika uandishi wa vichwa hivyo ambavyo vinaweza kuchunguzwa kwa mkabala wa kisintaksia. Hali hiyo imeibua ari ya kutaka kuchunguza udondoshaji wa vipashio hivyo na changamoto zake kwa wasomaji. Data za makala haya zilipatikana maktabani katika magazeti teule ya Kiswahili, yaani Mwananchi, Nipashe, Habari Leo na Uhuru kwa kutumia mbinu ya usomaji na uchambuzi wa matini. Data zilichambuliwa kwa kuzingatia mkabala wa kitaamuli wakiongozwa na Nadharia Rasmi ya Chomsky (1965). Matokeo ya utafiti uliozaa makala haya yanaonesha kwamba, vipashio vinavyodondoshwa katika uandishi wa vichwa vya magazeti ni visabiki vya vitenzi visoukomo, kiima cha sentensi tendwa, kiima cha sentensi tenda, vihusishi, viunganishi na vitenzi. Udondoshaji huu pamoja na kuonekana kama mtindo, vilevile wakati mwingine umeonekana kuwa na changamoto ya kuleta utata kwa msomaji.