Main Article Content
Utabirifu wa Makosa ya Utenganishaji na Uunganishaji wa Maneno katika Kiswahili
Abstract
Uandishi ni mchakato unaohitaji umakini ili kinachoandikwa kieleweke kwa msomaji kwa namna iliyokusudiwa na mwandishi. Ikiwa kueleweka kutazingatiwa, basi, kutakuwa na mawasiliano madhubuti. Hata hivyo, matini mbalimbali zimekuwa na makosa mengi kiasi cha kukwamisha mawasiliano baina ya mwandishi na msomaji wake. Lengo la makala haya ni kuchunguza utabirifu wa makosa katika uandishi kwa kumakinikia makosa ya utenganishaji na uunganishaji wa maneno. Nadharia ya Uchanganuzi Makosa ya Corder (1967) imetumika kuchambua na kujadili data za utafiti kwa sababu inahusika na makosa yanayohusiana na lugha na isimu. Data zimekusanywa kwa kutumia mbinu ya uchambuzi wa matini na usaili. Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba makosa ya kutenganisha na kuunganisha maneno yanatabirika kwa sababu yana uelekeo mmoja. Makosa ya kuunganisha maneno yamegawanyika katika makundi makubwa manne, yaani maneno yenye urejeshi, maneno yenye kiambishi cha umahali na wakati, maneno yanayotokana na uradidi, na maneno ambatani. Makosa ya kuunganisha maneno yamegawanyika katika makundi mawili ambayo ni mwambatano wa vitenzi shirikishi vya “kuwa na” na nomino, na viunganishi tegemezi vinavyoanza na “kwa”. Kwa ujumla, makosa haya yanatokana na uhamishaji wa kanuni moja katika uandishi wa maneno fulani yenye vipashio, hususani viambishi vinavyofanana. Kufuatia matokeo haya, makala haya yanapendekeza waandishi kuzingatia aina na sifa mahususi za maneno na si kujumuisha kanuni zinazotumika kuandika baadhi ya maneno.