Main Article Content
Mhusika Sauti katika Tamthilia ya Kimya Kimya Kimya ya Said A. Mohamed
Abstract
Makala haya yanalenga kudadisi sauti na uhusika wake kwenye uwasilishaji wa ujumbe katika tamthilia ya Kimya Kimya Kimya ya Said A. Mohamed (2011). Sauti kama mojawapo ya vipengele vya utendaji imetumiwa katika kazi tofautitofauti za tamthilia kwa sababu mbalimbali kutegemea mahitaji ya mtunzi wa kazi ya sanaa. Sauti inaweza kutekeleza jukumu kubwa inaposhirikishwa vilivyo katika tamthilia. Hata hivyo, watunzi wengi wanatumia sauti kwa ajili ya kushereheshea jambo fulani, kusisitizia ujumbe na kutoa maoni kuhusu wazo kuu linalolengwa hadhira. Wakati mwingine sauti huwa inatumika kama kicheko au kuweka utangulizi na kuhitimishia tamthilia. Kwa kuzingatia matumizi hayo, ni bayana kuwa matumizi ya sauti katika tamthilia nyingi bado hayajapewa uzito unaostahili. Kutokana na hali hiyo makala haya yanachunguza namna sauti ilivyotumika kama mhusika na uwasilishaji ujumbe kwa kurejelea tamthilia ya Kimya Kimya Kimya. Hivyo, mbinu iliyotumika kukusanya data za utafiti huu ni usomaji wa kina wa tamthiliya tajwa. Hii ni tamthilia ya kipekee katika matumizi ya sauti, ambapo mwandishi Said A. Mohamed amewajenga baadhi ya wahusika wake kama wahusika sauti. Amezifanya sauti sio tu kuongea bali pia kushiriki kikamilifu katika majibizano na uigizaji na wahusika wengine. Tumezingatia jinsi sauti ilivyotumika kujenga na kukuza wahusika na uhusika katika tamthilia ya Kimya Kimya Kimya kwa kujikita katika ushiriki wa mhusika binafsi, uhusika wa makundi na njia zinazotumiwa na wahusika sauti kuwasilisha ujumbe uliokusudiwa na mwandishi. Hatimaye, tumetathmini mchango wa sauti hizi katika kufanikisha utendaji na uwasilishaji maudhui kwa hadhira lengwa.