Main Article Content
Utabirifu wa kisemantiki wa mofimu {ji-} katika vitenzi vya Kiswahili
Abstract
Mofimu ni kipashio cha kimofolojia kinachobeba dhima za kisemantiki. Dhima hizo hutofautiana kutoka mofimu moja na nyingine kama mazingira ya utokeaji wa mofimu yanavyotofautiana. Katika lugha ya Kiswahili, baadhi ya vitenzi huwa na tabia ya kupachikwa mofimu ambazo hubeba dhima tofauti (Khamisi, 1985; Mgullu, 1999; McCarthy 2002; kwa kutaja wachache). Makala haya yanakusudia kuchunguza utabirifu wa kisemantiki wa mofimu {ji-] katika baadhi ya vitenzi vya Kiswahili ili kuona kama ni mara zote mofimu hiyo ikiambatana na vitenzi hivyo tunaweza kutabiri maana. Data iliyochambuliwa imekusanywa kutoka katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Toleo la tatu) na Kamusi Kuu ya Kiswahili (Toleo la pili), kwa kutumia mbinu ya usampulishaji nasibu tabakishi, usampulishaji nasibu taratibishi na usampulishaji nasibu ulo rahisi. Katika Makala haya tumeanza kwa kuangazia mbinu zinazobainisha vitenzi vyenye mofimu {ji-} katika kamusi teule za Kiswahili. Pia, tumefafanua utabirifu wa kisemantiki wa mofimu {ji-} katika vitenzi vya Kiswahili. Vilevile, tumeelezea mazingira yanayosababisha utabirifu wa kisemantiki wa mofimu {ji-} katika vitenzi vya Kiswahili. Ili kufikia malengo hayo, Nadharia ya Maana kama Matumizi imetumika. Kwa kuhitimisha, makala haya yametoa mapendekezo kadhaa kuhusu kufanyika kwa uchunguzi zaidi katika kipengele cha mofimu.