Main Article Content
Dhima ya methali kinzani
Abstract
Maadili katika jamii ni kipengele muhimu cha utamaduni na aghalabu huwasilishwa kupitia methali. Kimsingi, methali ni kauli za kifalsafa zinazotumiwa kuelezea na kuelekezea masuala kuhusu maisha ya wanajamii. Watu wanapozungumza, methali hujitokeza kama matini za ndani kwa ndani. Hivyo, methali hubeba ujumbe wa jumla unaohitaji kupatanishwa na miktadha ya kijamii. Mazingira haya huakisi mtazamo na tajiriba za jamii. Methali zinapotumiwa, huwa kurunzi ya kuukoleza zaidi ujumbe. Zinapotumika katika mazungumzo, matarajio ni kuibua jibu au tendo; kuonya kwa kuzingatia utamaduni wa jamii; kusuta matendo na kukemea matendo hasi ya watu. Katika uelekezaji wa maadili katika jamii, methali hutoa maelezo au kusuta kwa kuzingatia misimamo ‘mikali’. Methali hizo zimekuwa zikichukuliwa kwa ujumla kuwa zinapingana na zina mwelekeo hasi. Makala haya yanahakiki dhima ya methali kinzani katika kubainishia zaidi ujumbe wa kimaadili. Aidha, inabainishwa kuwa, methali zaidi ya moja zinaweza kutumiwa katika uwasilishaji wa ujumbe wa jumla na uelekezaji wa maadili katika jamii. Methali kinzani ni msingi katika kujengea mazingira ya uwajibikaji binafsi au wa kikundi cha watu.