Main Article Content

Ukubalifu wa tafsiri za kitamaduni: Mfano wa Tafsiri ya Filamu ya Yesu kutoka Kiingereza kwenda Kinyaturu


Rehema Stephano

Abstract

Makala haya yametathmini ukubalifu wa tafsiri za kitamaduni kwa kujiegemeza katika mswada wa tafsiri ya Filamu ya Yesu kutoka Kiingereza kwenda Kinyaturu. Utafiti uliozaa makala haya yameongozwa na Nadharia ya Skopos ya Hans J. Vermeer (1978) ambayo inazingatia lengo la kutafsiri matini lengwa. Utafiti huo pia umetumia mbinu mbili za kukusanyia data: uchambuzi wa matini na majadiliano ya vikundi lengwa, ambapo waigizaji wa sauti za Filamu ya Yesu ambao ni Wanyaturu tisa (9) wa umri wa miaka 40 - 80 walihusishwa katika majadiliano hayo. Matokeo ya utafiti yameonesha kuwa kuna vipengele vilivyokubalika kwa wazungumzaji wazawa wa Kinyaturu na vingine havikukubalika. Vipengele vilivyokubalika ni uzingatiaji wa tasifida katika kutafsiri miiko na urejeleaji wa wapendwa, yaani matumizi ya majina yanayosawiri hisia za upendo wakati wa kutafsiri. Vipengele vilivyokataliwa ni maneno yaliyopitwa na wakati, kutafsiri maneno kadhaa kwa kisawe kimoja, kutafsiri neno moja kwa visawe tofauti, na utohozi usio na sababu. Matokeo ya utafiti yameonesha zaidi kuwa utohozi wa maneno ya Kiswahili katika kutafsiri kwenda Kinyaturu unatokana na mtagusano wa Kinyaturu na Kiswahili, ambapo wazungumzaji wa Kinyaturu wanaonekana kuhamia katika Kiswahili na utamaduni wake. Makala haya yanaonesha kuwa utohozi huu ni kinyume na Nadharia ya Skopos ambayo tafsiri imekusudiwa ifanyike kwenda Kinyaturu kwa azma ya kuhifadhi lugha hiyo. Kwa upande wa vipengele ambavyo havikukubalika maboresho yalipendekezwa. Kufuatia matokea haya, makala haya yanapendekeza mfasiri kujua tamaduni za lugha chanzi (LC) na lugha lengwa (LL) kabla ya kufanya tafsiri yoyote ya kitamaduni ili kutoa tafsiri inayokubalika. Aidha, makala inasisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wazungumzaji wazawa wanaoishi eneo inapozungumzwa LL ili kuhakiki na kuiwezesha tafsiri ya kitamaduni kukubalika kwa wahusika.


Journal Identifiers


eISSN: 2546-2202
print ISSN: 0856-0129