Main Article Content
Ikolojia ya lugha nchini Tanzania na mustakabali wa lugha za jamii
Abstract
Makala haya yanahusu uchambuzi wa ikolojia ya lugha nchini Tanzania na mustakabali wa lugha za jamii. Lengo lake ni kuonesha jinsi Sera ya Lugha inavyotumika kujenga ikolojia kandamizi dhidi ya lugha za jamii nchini Tanzania. Data za utafiti zilitokana na mabango ya matangazo katika jiji la Mbeya na usaili na mamlaka zinazojihusisha na maamuzi kuhusu lugha na utamaduni. Data zote zimewasilishwa kwa mbinu ya ufafanuzi wa kinathari ili kurahisisha uelewekaji wake zinapohusishwa na Sera ya Lugha nchini Tanzania. Matokeo ya uchunguzi wa mabango ya matangazo 156 yanaonesha kuwa lugha zinazotumika katika matangazo ni Kiswahili na Kiingereza pekee. Data za usaili zinaonesha kwamba msimamo wa mamlaka za nchi ni kutoruhusu lugha za jamii kutumika katika maeneo ya umma kwa sababu ya kuzihusisha na ukabila, uvunjifu wa umoja wa kitaifa na kugawanyika kwa nchi. Tathmini ya Sera ya Lugha ya Tanzania kwa msingi wa Nadharia ya Kitaksonomia inadhihirisha itikadi ya kuziua lugha za jamii kwa lengo la kuimarisha utaifa. Itikadi hiyo inajitokeza waziwazi bila kuzingatia kwamba lugha za jamii ni muhimu katika maendeleo na ustawi wa jamii nzima. Pendekezo la makala haya ni kwamba mamlaka za lugha na utamaduni zifanye udurusu wa Sera ya Lugha ili kuhakikisha kuwa lugha zote zinapewa wigo mpana wa kutumika na kuhifadhiwa kwa faida za watumiaji wake na makuzi endelevu ya lugha ya Kiswahili.