Main Article Content

Dhima ya Sadfa ya Kimapenzi katika Kujenga Matukio ya ‘Kishushushu’ na ‘Kijasusi’: Uchunguzi wa Riwaya ya Kikosi cha Kisasi


Gervas A. Kasiga
Eliamini M. Maffa

Abstract

Shabaha ya makala haya ni kufafanua matumizi ya sadfa ya kimapenzi katika kuwasaidia watunzi kujenga tungo mbalimbali za kisanaa na kutimiza au kukamilisha uwasilishaji wa matukio ya kishushushu na kijasusi. Ufafanuzi wetu umemakinikia riwaya ya Kikosi cha Kisasi ya mwandishi Aristablus Elvis Musiba. Sadfa ni hali ya utokeaji wa matukio kwa wakati mmoja kwa namna inayoshangaza au inayoashiria bahati. Hii ni miongoni mwa mbinu zinazotumiwa na watunzi katika kuzijenga na kuzikamilisha tungo zao (Wamitila, 2003; Dannenberg, 2008). Mara nyingi watunzi wa kazi za kifasihi huitumia mbinu hii sambamba na mbinu nyingine katika kufanikisha azma ya tungo hizo. Mbinu hizo nyingine zaweza kuhusisha uhalisiajabu, utanzia, ufutuhi, na usemezano. Kazi ya kifahisi hujengwa kwa kutumia mbinu mbalimbali za kisanaa zinazoafikiana na lengo pamoja na aina ya kazi ya kifasihi inayowasilishwa. Sadfa ni mojawapo ya mbinu hizo za kisanaa ambayo hutumiwa na watunzi kuibua, kujenga na kukamilisha azma ya tungo zao. Katika mjadala wa makala haya tumeonesha namna sadfa ya kimapenzi ilivyotumika kwenye miktadha ya kutiana moyo wa kufanikisha kazi ya kishushushu na kijasusi; kuleta urahisi wa ufanikishwaji wa kazi ya kishushushu na kijasusi; kusaidia uokozi na uchocheaji kisasi; na mwishowe kusababisha uvumbuzi wa taarifa muhimu za kijasusi pamoja na ukamilishwaji wa operesheni za kijasusi. Katika riwaya teule mwandishi ameitumia mbinu hii kupitia mahusiano ya kimapenzi baina ya mhusika wake mkuu Willy Gamba (mwanamume) pamoja na wahusika wasaidizi (mabinti) Amanda, Ntumba, Mwadi na Tete.


Journal Identifiers


eISSN: 2546-2202
print ISSN: 0856-0129