Main Article Content
Usanaa wa Lugha katika Ujenzi wa Dhima za Nyimbo: Mfano Kutoka Nyimbo za Harusi za Jamii ya Waasu
Abstract
Nyimbo ni utanzu muhimu wa fasihi simulizi unaopatikana katika jamii mbalimbali za wanadamu. Zipo nyimbo za aina mbalimbali, miongoni mwazo ni nyimbo za harusi zinazotumika katika sherehe za ndoa (Wamitila, 2004). Nyimbo hizi zina dhima muhimu inayofungamana na sherehe ya harusi, hususan kwa maharusi. Kwa kawaida nyimbo haziimbwi chapwa, bali huhusisha usanaa wa lugha na mbinu nyingine za kiutendaji. Makala haya yanajadili usanaa wa lugha katika nyimbo za harusi miongoni mwa jamii ya Waasu. Usanaa wa lugha huzifanya nyimbo kuvutia na kuwa na athari chanya kwa walengwa wake (Perpetua, 2011). Waasu ni jamii inayopatikana Kaskazini Mashariki mwa Tanzania, katika wilaya za Same na Mwanga, mkoani Kilimajaro (Mreta, 2008). Jamii hii inazo nyimbo anuwai zinazoimbwa katika sherehe mbalimbali. Miongoni mwazo ni nyimbo za harusi zinazoimbwa kwenye sherehe ya harusi. Nyimbo hizi huimbwa kwa kutumia lugha ya Chasu. Uimbwaji wake hauambatani na uchezaji wala matumizi ya ala za muziki. Nyimbo za harusi katika jamii ya Waasu hutumia usanaa wa lugha katika kujenga dhima zake. Matokeo ya utafiti wa makala haya yanaonesha kwamba zipo mbinu mbalimbali za usanaa wa lugha, kama vile: jazanda, maneno teule, dhihaka, tashbiha, chuku na takriri, zinazotumika katika ujenzi wa dhima za nyimbo za harusi za jamii ya Waasu. Mbinu hizi huzifanya nyimbo hizo kuvutia, kufikirisha na kuleta hamasa na hamu ya kuzisikiliza. Kwa kufanya hivyo, walengwa huupata ujumbe uliokusudiwa kwa uzito stahiki. Kutokana na matokeo hayo, jamii mbalimbali zinahamasishwa kudumisha nyimbo zake za kijamii ili kuendeleza amali za kijamii.