Main Article Content
Mikabala ya Uchanganuzi wa Viambajengo vya Sentensi na Istilahi Zinazotumika: Mifano kutoka Lugha ya Kiswahili
Abstract
Uchanganuzi wa viambajengo vya sentensi unaweza kufanywa kwa kutumia mikabala mbalimbali . Kila mkabala unaambatana na matumizi ya istilahi zake mahususi . Licha ya kuwapo kwa mipaka ya istilahi hizo, bado kuna uchanganyaji wa matumizi yake. Uchanganyaji huu unaashiria kwamba mikabala ya uchanganuzi wa viambajengo vya sentensi na istilahi zinazohusika ni masuala ambayo hayako wazi sana miongoni mwa wanaisimu. Hivyo, makala haya yanahusu mikabala ya uchanganuzi wa viambajengo vya sentensi na istilahi zinazohusika kwa kutumia mifano kutoka lugha ya Kiswahili. Data za makala haya zimepatikana kwa njia ya hojaji, usaili na uchambuzi matini. Ufafanuzi wa data umeongozwa na misingi ya N adharia ya Sarufi Leksia Amilifu ya Bresnan na Kaplan (ya mwishoni mwa miaka ya 1970). Matokeo yanaonesha kwamba viambajengo vya sentensi vinaweza kuchanganuliwa kimuundo, kiua milifu, kisemantiki na kipragmatiki. Kwa kuzingatia mikabala hii kuna istilahi za kimuundo, kiuamilifu, kisemantiki na kipragmatiki. Kwa ujumla makala haya yanahitimisha kwamba istilahi za uchanganuzi wa viambajengo vya sentensi hazitumiki kiholela bali huamuliwa na m i kabala ya uchanganuzi wa viambajengo.