Main Article Content

Korasi katika Filamu za Kiswahili


Selestino H. Msigala

Abstract

Baadhi ya wahakiki kama vile Mulokozi (1996), Mbonde (2002), Wamitila (2008) na Njogu na Chimerah (2011) wamehakiki kazi za fasihi kwa kutenganisha vipengele vya fani na vya maudhui. Mkabala wa kuchambua fasihi kwa kujiegemeza katika ama fani au maudhui umezoeleka na umekuwa ukitumiwa na wataalamu wengi. Hata hivyo, kama alivyoeleza Mutembei (1995, 2012), utenganishaji wa fani na maudhui ni wa kidhahania tu, kwani misingi ya fani na maudhui kwa dhati yake haitenganishiki. Ili kuyakabili masuala ya kifani na kimaudhui kwa pamoja, bila kuyatenganisha palihitajika nadharia mwafaka itakayotumika kuhakiki kazi za kifasihi bila kutenganisha vipengele hivyo. Mutembei (2012) aliiasisi na kuiita Nadharia ya Korasi. Hata hivyo, wataalamu waliotangulia kushughulikia korasi kama vile: Weiner (1980), Whalley (1997), Abraham (1999), Morgan na Olaniyan (2004), Storey na Allan (2005), Schlegel (H.m) na Mutembei (1995, 2012) wameitumia nadharia hii zaidi katika fasihi andishi (tamthilia, riwaya na ushairi). Matumizi ya nadharia hii katika uchambuzi wa kazi za kifasihi zinazohusiana na tanzu hizo yalionesha kwamba korasi inaweza kujitokeza kama dhamira, tukio la kijamii, mhusika, kimya, wimbo, muundo na tukio la mila na desturi. Jambo ambalo halijajulikana linaloshuhulikiwa katika makala haya ni namna nadharia hii inavyoweza kutumika katika fasihi simulizi ya kidijiti, yaani filamu. Makala yamelenga kuchambua matumizi ya nadharia husika katika kazi ambazo ni za kiutendaji zaidi, yaani hazitegemei sana maandishi. Tunadadisi, je, ujitokezaji wa vipengele vya kikorasi utakuwa uleule kama katika tamthilia zilizoandikwa au kunaweza kuwapo na mabadiliko? Kwa maneno mengine, je, korasi inawezaje kujitokeza katika kazi za kifasihi katika ujumla wake? Kwa kutumia filamu kama utanzu wa fasihi simulizi ambayo inawasilishwa kwenye media mbalimbali za kidijiti (filamu), makala haya yanalenga kujadili wazo hili. Katika uchambuzi wetu tumetumia filamu ya “Chausiku”.


Journal Identifiers


eISSN: 2546-2202
print ISSN: 0856-0129