Main Article Content

Ulinganishi wa Mfumo wa Ngeli za Nomino katika “Lugha” za Kibantu za Mara Kaskazini


Alphonce B. Morango

Abstract

Makala haya yanahusu uchunguzi wa mfumo wa ngeli za nomino katika “lugha2” zilizo Kaskazini mwa mkoa wa Mara ambazo ni Kikurya, Kisimbiti, Kikiroobha, Kisweeta, Kikabwa, Kisuba1, Kikine na Kikenye. Mkoa huu una lugha nyingi ambazo zinafanana, ingawa wazungumzaji wake wanadai wanazungumza lugha tofauti. Makala haya yanachunguza mfanano na tofauti za mfumo wa ngeli katika “lugha” za Kibantu za Mara Kaskazini. Nadharia inayoongoza uchunguzi wa mfumo huu ni “Nadharia ya Isimu Historia-Linganishi” iliyoasisiwa na mwanaisimu William Jones (1786). Msisitizo mkubwa wa nadharia hii ulikuwa kulinganisha lugha kwa lengo la kufanya uundaji upya wa lugha ya awali. Data zilizotumika katika makala haya zimepatikana kutoka uwandani, ambapo wazungumzaji wa lugha hizo wanapatikana. Utafiti ulitumia mbinu za kusikiliza, usaili, hojaji na majadiliano kwenye majopo katika ukusanyaji wa data. Aidha, mbinu ya kikompyuta ilitumika katika uchanganuzi wa data. Matokeo ya utafiti yanadhihirisha kuwa kuna mfanano mkubwa wa “lugha” hizi wa takribani asilimia sabini na saba (77%). Hivyo, hizi si lugha zinazojitegemea bali ni lahaja ambazo zimetokana na lugha moja kuu ya awali na kugawanyika katika makundi mawili: kundi moja linahusisha Kikurya, Kisimbiti, Kikiroobha, Kisweeta, Kikine, na Kikenye. Kundi la pili lina lugha za Kisuba na Kikabwa.


Journal Identifiers


eISSN: 2546-2202
print ISSN: 0856-0129