Main Article Content
Kupokelewa Zaidi Kwa Simu Ya Mkononi Kuliko Kompyuta Na Athari Zake Kwa “Waswahili” Wa Afrika Mashariki
Abstract
Mtandao wa tovuti ni nyenzo ya msingi katika maendeleo ya uwanja wa mawasiliano unaounganisha watu na jamii mbalimbali katika ulimwengu wa leo unaotandawaa. Katika “ulimwengu wa kwanza na wa pili”, yaani mabara ya Amerika, Uropa na Asia, maendeleo na mapinduzi makubwa katika uwanja wa teknolojia ya mawasiliano yanategemea kompyuta kama chombo cha msingi cha matumizi ya mtandao huu. Hali hii ni tofauti sana katika mapinduzi ya teknolojia ya mawasiliano katika Afrika. Kupokelewa na kusambaa kwa simu za mkononi kumeibuka na kushika kasi sana; si tu katika uwanja wa mawasiliano, bali pia katika utangamano na uhusiano kati ya watu binafsi na kati ya makampuni ya biashara na taasisi za umma. Katika mapinduzi haya, shughuli za mawasilliano, biashara, uchumi na ubadilishanaji wa pesa zinatumia mtandao wa simu mkononi. Kwa mfano, kuibuka kwa huduma ya kuweka, kutuma na kutumia pesa ya M-pesa kumebadlisha dhana ya jadi ya biashara na utamaduni wa huduma za benki. Makala haya yanachunguza asili, sababu na matokeo ya mtandao huu wa simu za mkononi katika utamaduni mpya wa kimawasiliano na kibiashara kati ya wananchi wa Afrika Mashariki na kati ya Afrika Mashariki na ughaibuni. Katika uchunguzi huu, makala yanahitimisha kwamba ijapokuwa kusambaa kwa simu za mkononi kumechangiwa na urahisi wa gharama, matumizi na kuenea kwa mtandao wa simu hizi, kukubalika na kupokelewa kwake haswa na “Waswahili” – wananchi wa kawaida wa Afrika Mashariki - kunatokana na namna ambavyo matumizi yake yanamsaidia Mwafrika kuishi katika utamaduni wake wa kimaongezi, tofauti na mitandao inayotegemea kompyuta inayowalazimisha Waafrika kushadidia utamaduni wa maandishi ambao ni mgeni Uswahilini. Hili limemwezesha Mswahili si tu kuipokea simu ya mkononi kwa mikono miwili, bali pia kuiswahilisha na kuinasibisha na utamaduni wake kwa matokeo ambayo yameleta mapinduzi makubwa kwa maisha yake