Main Article Content
Athari Na Dhima Ya Vijenzi Nomino Katika Vitenzi Vya Kiswahili
Abstract
Unyambulishi ni mchakato wa uundaji wa maneno kwa kutumia vijenzi au vinyambulishi mbalimbali. Katika mchakato huu wakati mwingine neno huhama kutoka kategoria yake na kuingia katika kategoria nyingine. Mathalani, kivumishi kinaweza kubadilika na kuwa kitenzi au kitenzi kuhama kategoria yake na kuwa nomino. Ujenzi au uundaji wa maneno ni mchakato muhimu sana katika lugha. Uundaji wa maneno husaidia kuongeza msamiati wa lugha inayohusika kupitia kuunda istilahi na maneno kwa ajili ya dhana mpya. Sambamba na dhima yake ya ukuzaji wa lugha kimsamiati, vinyambulishi hivi vina athari mbalimbali kimofofonolojia na pia vina dhima maalumu kisemantiki.
Makala haya yanachambua na kufafanua athari na dhima ya vijenzi nomino katika lugha ya Kiswahili. Makala yanajaribu kuchambua athari za kimofofonolojia, katika mizizi au mashina ya vitenzi vya Kiswahili, zinazotokana na upachikaji wa vijenzi nomino. Makala yanaonyesha jinsi sauti za mwisho katika mizizi au mashina ya vitenzi zinavyoathiriwa na vijenzi nomino na kusababisha mabadiliko ya umbo la mzizi au shina la kitenzi. Uchambuzi wa athari za kimofofolojia unaongozwa na taaluma ya mofolojia ya leksika inayohusu viambishi vyenye athari na visivyo na athari. Mkabala huu unaamini kwamba katika michakato ya kimofolojia kuna viambishi vinavyosababisha athari fulani za kimofofonolojia na vingine havina athari hiyo. Makala haya yamebainisha vijenzi nomino vya Kiswahili vyenye athari na visivyo na athari. Halikadhalika, makala yanaeleza dhima mbalimbali za kisemantiki zinazotokea baada ya nomino inayoundwa kupachikwa viambishi ngeli. Makala yanabainisha kwamba nomino inayoundwa (nomino-unde) huwa na maana tofauti kulingana na aina ya ngeli inayopachikwa mwanzoni mwa nomino hiyo. Kutokana na hali hii ni muhimu kwa kila nomino-unde kuambikwa kiambishi ngeli ili iwe na maana inayojitosheleza.