Main Article Content

Mkabala Wa Ki-Korasi Katika Kuchambua Kazi Za Fasihi Ya Kiswahili: Mifano Kutoka Katika Tamthiliya


AK Mutembei

Abstract

Kwa wachambuzi na wahakiki wa fasihi ya Kiswahili, mtazamo umekuwa ni wa kugawa makundi mawili: fani na maudhui. Hata hivyo, karibu wote wanakubaliana kuwa mgawanyo huu ni wa kinadharia zaidi na unafanyika kwa ajili ya uchambuzi na uhakiki;  kwani katika hali halisi maudhui huwezi kuyatenga kutoka katika fani (Senkoro 1982). Ingawa hivi ndivyo inavyojulikana, hakuna aliyeweza kupendekeza njia ya uchambuzi itakayoziweka pamoja dhana za maudhui na fani. Kwangu mimi, tatizo liko katika umapokeo, na kwa hiyo wachambuzi na wahakiki ambao bado wanashikilia dhana za fani na maudhui kwamba ndizo pekee zitumikazo katika uchambuzi wa fasihi wamegubikwa na mazoea ya kimapokeo ambayo mara nyingi hugomea mabadiliko. Dhana za fani na maudhui zimesimama kama sheria-mama katika uchambuzi na uhakiki wa fasihi. Kutokana na mtazamo huu wa ki-fani na ki-maudhui, wahakiki na wachambuzi wa fasihi kama vile tamthilia wameweka vigezo ambavyo havina budi vifuatwe iwapo mtu atataka kuichambua na kuihakiki kazi ya fasihi. Vigezo hivi sasa vimechukuliwa kama ni sheria katika uchambuzi na uhakiki wa tamthilia. Hata kuna waliothubutu kuweka "sheria" katika ubunifu wa kazi za fasihi Lakini uchambuzi, na hata uhakiki, kama ulivyo utunzi wa kifasihi, ni vigumu kuubana kwa sheria kama hizo. Suala la sheria katika usanii linaelekea kuwa jadi ya wanamapokeo (Abedi 1954; Mayoka 1984). Jambo hili limepingwa vikali katika usanii wa ushairi wa Kiswahili (Kezilahabi 1974; Mulokozi na Kahigi 1979). Likapingwa na E. Hussein kuhusu tamthilia aliposema: "Kuandika mchezo wa kuigiza ni kuumba sanaa. Na sanaa hukataa maelezo; kamwe haitaki sheria" (Hussein 1983: 195). Katika makala haya linapingwa katika uchambuzi wa fasihi ya Kiswahili. Nasisitiza kuwa fani na maudhui zisichukuliwe kuwa ndio dhana pekee zinapopaswa kuangaliwa wakati wa kuchambua fasihi. Dhana ya korasi ikieleweka vizuri, itaonekana kuwa ni kipengele kinachopaswa kuangaliwa kwa upekee wake na kikatumika katika uchambuzi wa kazi ya fasihi.


Journal Identifiers


eISSN: 0023-1886