Main Article Content
Dhima ya Visasili katika Riwaya za Nagona na Mzingile
Abstract
Nagona na Mzingile ni riwaya zilizoibua mjadala mkubwa katika fasihi ya Kiswahili. Upekee wa riwaya hizo umewasukuma wataalamu wengi kuandika mengi kuhusiana nazo. Makala hii imechangia katika mjadala huo kwa kuvishughulika visasili vilivyomo katika riwaya hizo. Kwa hiyo, malengo ya makala hii ni kuvibainisha visasili hivyo kisha kujadili dhima yake katika riwaya teule. Makala ilihusisha usomaji wa riwaya tajwa kabla ya kuanza kuvichambua visasili vilivyoshughulikiwa. Ili kukamilisha malengo yake, makala imetumia nadharia mbili, yaani Nadharia ya Mwingilianomatini na Nadharia ya Uhemenitiki. Nadharia ya Mwingilianomatini imetumika wakati wa kuvibainisha visasili katika riwaya za Nagona na Mzingile. Pia, Nadharia ya Uhemenitiki imetumika wakati wa kujadili dhima za visasili katika riwaya teule. Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa katika riwaya ya Nagona kuna kisasili cha Edipode, kisasili cha manju wa ngoma ya uhai na kisasili cha mama na kijana wake. Kwa upande wa riwaya ya Mzingile, kuna kisasili cha Kakulu na kisasili ya Adamu na Hawa. Aidha, tumebaini kuwa visasili vilivyotumika katika riwaya za Nagona na Mzingile vina dhima ya kujenga uhalisiaajabu katika riwaya tajwa, kuleta tafsiri anuwai za riwaya husika na kujenga maudhui kuhusu ukweli, asili na maana ya maisha.