Main Article Content
Faida ya Kujifunza kwa Kuegemea Mfumo wa Isimu ya Kiswahili: Mfano wa China
Abstract
Makala3 hii inachunguza changamoto na faida zilizopo kwa wanaojifunza Kiswahili kwa kutumia mifumo ya kiada iliyopo nchini China. Mifumo hii inaweza kujumuishwa katika makundi mawili4 . Kundi la kwanza ni mfumo ulioenea nchini China, kama maeneo mengine ulimwenguni, ambao hugawa nomino katika umoja na wingi kama kielelezo kikuu. Kundi la pili ni mfumo ambao umetungwa kwa kuiegemea isimu ya Kiswahili na ya lugha yake mame ya Kibantu. Data zilikusanywa uwandani kwa njia ya hojaji na mahojiano ya ana kwa ana. Mbinu zilizotumika katika uchanganuzi wa data ni mkabala wa kimaelezo. Uchambuzi uliongozwa na Nadharia ya Uamilifu. Matokeo yanaonesha kuwa mfumo ulioenea China si tofauti na ule ulioanzishwa nyakati za ukoloni, wakati ambapo mfumo wa isimu ya Kiswahili haukutambulika na hata manufaa yake katika utunzi wa mitaala na vitabu vya Kiswahili hayakutiliwa maanani. Ingawa hali hii huonekana kama inawafaa wanaoanza kujifunza Kiswahili angalau mwanzoni, baada ya muda mfupi huwa bayana kuwa baadhi ya masuala yanayofundishwa katika lugha hii hayaelezeki kwa njia mwanana kimfumo.