Main Article Content
Ubainishaji wa ‘Sura Mbili’ katika Methali za Kiswahili
Abstract
Tafiti mbalimbali zimewahi kufanywa kuhusu methali za Kiswahili. Tafiti hizo zimejikita mno kwenye fasiri za maana, fafanuzi, uainishaji na maelezo ya kijumla. Juhudi hizo za awali zinaashiria kuwa, methali za Kiswahili ni ‘jungu kuu’ na zinahitaji uhakiki na utafiti wa kina. Kutokana na umuhimu wake katika jamii, zimekuwa zikipokezwa kimuktadha kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Kwa maana hii, zimekuwa ni vito vya kuhifadhi na kuwasilisha busara zinazojikita katika falsafa za jamii. Aidha, zimekuwa zikitumika zaidi katika ubainishaji na uelekezaji wa masuala muhimu ya jamii. Maelezo ya kijumla yamekuwa yakitolewa kuhusu methali hizo kwamba, ni ‘kauli fupi’ za kimapokeo. Huo ni uegemeo unaojikita kwenye sifa za kimuundo na kimaumbo. Mwelekeo huo hausaidii sana katika ubainishaji wa busara katika jamii husika. Kutokana na jinsi methali za Kiswahili zinavyotumiwa katika jamii, kuna namna mbili zinazojitokeza: ufupi na urefu wake. Nadharia ya Semiotiki imetumika katika kufafanulia sura hizo mbili kwa kuzingatia miktadha ya kijamii.