Main Article Content
Mchango wa Ngonjera katika Kuchochea Harakati za Ukombozi wa Utamaduni wa Mwafrika: Mifano kutoka Ngonjera za Ukuta II
Abstract
Miongoni mwa masuala yaliyowashughulisha watunzi wa kazi za fasihi baada ya uhuru ni pamoja na suala la ukombozi wa kiutamaduni. Suala hili halikuepukika kwa sababu ujio wa wageni katika bara la Afrika ulifungamana na mambo muhimu matatu. Mosi, kuhifadhi baadhi ya masuala waliyoona yana tija kwao. Pili, kuharibu baadhi ya masuala waliyoyakuta Afrika. Tatu, kuanzisha masuala mapya. Utamaduni wa Mwafrika ni miongoni mwa mambo yaliyoharibiwa kwa kuingiziwa vipengele vya tamaduni za kigeni. Baada ya uhuru wa nchi za Kiafrika, hatua iliyofuata ilikuwa kupigania ukombozi wa utamaduni. Mathias Mnyampala ni miongoni mwa watunzi ambao hawakubaki nyuma katika kuchochea harakati hizi za ukombozi wa utamaduni wa Mwafrika. Katika kufanikisha kuonesha namna ambavyo Mathias Mnyampala hakubaki nyuma katika kudhihirisha harakati za ukombozi wa utamaduni wa Mwafrika, tunatarajia kutumia Nadharia ya Ubaadaukoloni. Tutatumia nadharia hii kwa kuwa ndio nadharia inayoonekana kuangazia vema masuala yanayohusiana na harakati za ukombozi wa Mwafrika kifikra baada ya ukoloni.