Main Article Content
Dhana za “Junzi” na “Xiaoren” katika Fasihi Andishi: Utafiti Linganishi wa Wahusika katika Fasihi za Kiswahili na Kichina
Abstract
Kutokana na maendeleo makubwa ya utandawazi duniani kote, tamaduni za sehemu mbalimbali duniani zinajulikana siku baada ya siku. Jamii za Asia na Afrika, kama zilivyo jamii nyingine, zinakua kwa kasi huku zikiakisi polepole mazingira ya tamaduni mbalimbali za kutoka maeneo mengine ya dunia. Wakati huohuo, zinajiunda upya katika upeo wa utamaduni wa kisasa. Fasihi, kama mojawapo ya njia kuu za mawasiliano, hutoa mchango muhimu katika mawasiliano ya tamaduni tofauti. Kwa mantiki hiyo, utafiti huu unalinganisha fasihi za tamaduni za Kiswahili na Kichina ili kuchunguza mawasiliano baina ya tamaduni hizi mbili. Bila shaka, utafiti huu utawasaidia watafiti kuelewa kufanana na kutofautiana kwa fasihi na tamaduni hizi kwa kina zaidi. Fasihi ya Kiswahili na ile ya Kichina zilianza zikaendelea na kukomaa katika jamii tofauti na vipindi tofauti. Kwa hiyo, historia zao hazifanani kabisa. Hata hivyo, katika baadhi ya kazi, fasihi hizi zinabeba falsafa zinazofanana. Makala hii inachunguza wahusika wa hadithi fupi ya Kiswahili iitwayo “Kunani Marekani?” na wa riwaya ya Kichina Ndege Mvumaji2 wa Los Angeles(洛杉洛杉矶蜂鸟. Lengo la makala hii ni kuonesha jinsi dhana ya “Junzi-Xiaoren” (muungwana na mtu wa kawaida) inavyojenga mazingira katika fasihi tofauti na kufungua dirisha la mawasiliano ya fasihi ya Kiswahili na ya Kichina. Katika makala hii, mtafiti ametumia Nadharia ya Utafiti Sambamba wa Fasihi Linganishi (Parallel Research of Comparative Literature) ili kuzilinganisha kazi kutoka katika tamaduni tofauti kabisa ambazo hazijadhaniwa kufungamana tangu zamani.