Main Article Content

Dhana ya Vina na Mizani na Dhima yake katika Ushairi wa Kisasa wa Kiswahili


Aldin Mutembei

Abstract

Katika makala hii, tunajadili dhana ya vina na mizani na kuhakiki dhima yake kama inavyojitokeza katika shairi la Kiswahili. Katika kufanya hivi, tumehakiki mitazamo ya pande mbili ambazo mwishoni mwa miaka ya 1960 ziliibua makundi mawili yaliyozusha mjadala mkali kuhusiana na maana ya ushairi wa Kiswahili. Kundi la kwanza linajulikana kama wanamapokeo. Kundi hili lilishikilia kuwa urari wa vina na mizani na kuimbika kwa shairi ni vipengele vya lazima katika kuufanya utungo uwe shairi la Kiswahili; na kundi la pili lilikuwa na mtazamo kuwa vipengele hivyo si vya lazima, na kuwa si lazima ushairi wa Kiswahili uimbike. Kundi hili linajulikana kama wanamabadiliko (au wanausasa). Makala inajadili na kupendekeza mtazamo mwingine wa kuviangalia vina na mizani katika shairi la Kiswahili. Katika makala hii, tumetumia Nadharia ya Mwitiko wa Msomaji ili kujadili maana aipatayo msomaji wa shairi la Kiswahili kuhusiana na vina na mizani. Makala imejibu maswali mawili: Je, kuna namna moja ya kuangalia maana ya vina na mizani? Je, inawezekana kuwa na vina na mizani katika shairi lisiloimbika? Makala inahitimisha mjadala kwa kudai kuwa ikiwa makundi yote mawili yangeangalia vipengele hivi kiuamilifu, yangefikia uamuzi unaofanana au angalau kukaribiana kuhusiana na nafasi ya vina na mizani
katika shairi la Kiswahili. Kwa mantiki hiyo, labda kusingejitokeza mgogoro wa ushairi kama uliotokea.


Journal Identifiers


eISSN: 0023-1886