Main Article Content
Upinduzi wa Kimahali katika Lugha ya Kiswahili: Dhima za Kisarufi na Sifa za Kimofosintaksia za Viambajengo Vinavyohusika
Abstract
Ingawa mchakato wa upinduzi wa kimahali umefanyiwa utafiti katika lugha mbalimbali za Kibantu, dhima za kisarufi za viambajengo vinavyohusika hutofautiana kati ya lugha moja na nyingine. Pamoja na kutofautiana huko, pia kuna utata wa dhima hizo. Mathalani, Salzman (2004) anaeleza kuwa kithimu kilichopinduliwa ni yambwa na, kwa upande mwingine, anaeleza pia kwamba kithimu hicho siyo yambwa. Hivyo, haikubainishwa wazi kama kithimu hicho ni yambwa au siyo yambwa. Pia, kama siyo yambwa, haikuwekwa wazi kwamba kina dhima gani. Lengo la makala hii ni kubainisha viambajengo vinavyohusika katika upinduzi wa kimahali, dhima za kisarufi za viambajengo hivyo pamoja na sifa zake za kimofosintaksia katika Kiswahili. Makala inabainisha kwamba viambajengo vinavyohusika ni kimahali, kithimu, na mtenda. Aidha, kimahali kisichopinduliwa ni oblikyumahali na, kile kilichopinduliwa ni kiima; kithimu kisichopinduliwa ni kiima na kile kilichopinduliwa ni yambwaθ; na mtenda asiyepinduliwa ni kiima na yule aliyepinduliwa ni chagizo. Hitimisho la makala hii ni kwamba viambajengo vinavyohusika katika upinduzi wa kimahali vinadhihirisha mabadiliko ya dhima za kisarufi. Data za makala hii zimekusanywa kwa mbinu ya upitiaji wa nyaraka (Whiteley, 1968; Mkude, 2005; na Khamis, 2008) na ushuhudiaji-shiriki. Ufafanuzi wa data umeongozwa na Nadharia ya Sarufi Leksia Amilifu ya Bresnan na Kaplan (mwishoni mwa miaka ya 1970).