Main Article Content
Maendeleo ya Fasihi ya Kiswahili ya Watoto nchini Tanzania na Kenya: Mkabala Linganishi
Abstract
Fasihi ya Kiswahili ya watoto kama taaluma haina muda mrefu katika historia ya fasihi ya Kiswahili. Ikilinganishwa na fasihi ya watu wazima ambayo ilianza muda mrefu, na pia tafiti nyingi kufanyika katika mataifa mengi, fasihi ya watoto inaonekana kuwa imetelekezwa kwa muda mrefu kutokana na kutokupewa umuhimu unaostahili na wahakiki na hivyo kudharauliwa na wanajamii (Bakize, 2013). Wanajamii wengi wamekuwa wakiinasibisha fasihi hii na mambo ya kitoto ambayo ni rahisi, yasiyo ya msingi sana; na ndiyo maana inaitwa fasihi ya watoto (Wamitila, 2008). Tafiti zinaonyesha kwamba fasihi hii imechipuka barani Afrika hivi karibuni, hasa kwenye miaka ya 1980 kutokana na sababu kadhaa lakini mojawapo ikiwa ni kutiliwa mkazo kwa masuala ya haki za watoto (Ngugi, 2016a). Mulokozi (katika Semzaba, 2008) anaeleza kwamba nchini Tanzania, fasihi ya watoto ilichipuka wakati na baada ya ukoloni katika miaka ya 1960 na kushika mizizi miaka ya 1970. Zaidi ya hayo, fasihi hii ilishika mizizi zaidi miaka ya 1990 baada ya kuzinduliwa kwa mradi wa Vitabu vya Watoto Tanzania. Mradi huo uliwawezesha waandishi, wachapishaji na wachoraji wa vitabu vya watoto kufanya kazi za fasihi ya watoto kwa weledi zaidi. Aidha, mradi pia ulifungua maktaba katika shule zilizo chini ya Mradi huo na kusambaza vitabu vilivyochapishwa kwa ajili ya usomaji wa ziada. Hadi kufikia mwaka 2015, mradi umewezesha uchapishaji na usambazaji mashuleni vitabu zaidi ya 350 (CODE, 2015). Nchini Kenya, fasihi ya watoto imepata umaarufu miaka ya 2000 baada ya kujumuishwa katika somo la Kiswahili kuanzia shule ya msingi hadi sekondari. Vilevile, hatua ya serikali ya kugharimia masomo imechangia vikubwa katika maendeleo haya kwa sababu serikali ilichukua jukumu la kununua vitabu vya ziada na kiada. Makala haya yanalenga kutathmini maendeleo ya fasihi ya Kiswahili ya watoto kwa kufanya ulinganishi katika nchi za Tanzania na Kenya. Nchi hizi zimeteuliwa kwa sababu, kwa mujibu wa utafiti wa awali, fasihi ya Kiswahili ikiwa ni pamoja na fasihi ya watoto ya Kiswahili imepamba moto zaidi katika nchi hizi mbili za Afrika Mashariki kuliko nchi nyingine.