Main Article Content

Majukumu ya Wahusika Wanawake katika Tendi teule za Kiswahili


Wendo Nabea
Jackson Ndung’u

Abstract

Utendi ni mojawapo ya tanzu za fasihi ya Kiswahili ulio na historia ndefu. Miongoni mwa tendi hizi ni Utendi wa Mwanakupona, Utendi wa Fumo Liyongo, Utendi wa Swifa ya Nguvumali, Utendi wa Ngamia na Paa, na Utendi wa Mikidadi na Mayasa au Utendi wa Qiyama. Tendi hizi huwa na sifa zinazolandana upande wa maudhui, fani na hata muundo. Mojawapo ya sifa zinazofungamana na tendi za Kiswahili, sawa na tendi nyingine za mataifa mengine, ni kuwa kazi za kishujaa. Wahusika wakuu huaminika ni mashujaa madhali huwa wametenda mambo ya kufaa familia, jamii na hata mataifa yao. Hata hivyo, ushujaa katika tendi za Kiswahili hufungamanishwa na wahusika wa kiume, japo tendi zina wahusika wa kike pia. Makala haya yaliyojikita katika Ufemenisti, Mkabala wa Kiafrika, yanadhihirisha kuwa wanawake wana majukumu muhimu, yakiwemo yale yanayofungamana na ushujaa, lakini ambayo wasomi hukosa kuyatambua. Hili litabainishwa kupitia matokeo ya uchunguzi wa majukumu ya wahusika wanawake katika tendi teule za Kiswahili. Makala yatatumia Utendi wa Fumo Liyongo, Utendi wa Mikidadi na Mayasa na Utendi wa Sifa ya Nguvumali. Kazi hii itaziba pengo kuhusiana na wajibu wa wanawake katika tendi za Kiswahili, hasa kuhusiana na ushujaa.

Journal Identifiers


eISSN: 0023-1886