Main Article Content
Riwaya ya Kiswahili katika ufundishaji wa historia
Abstract
Makala haya yanachunguza uwezekano wa riwaya ya Kiswahili kutumika katika ufundishaji wa historia. Makala yamejiegemeza katika kuonesha namna ambavyo riwaya kama utanzu mmojawapo wa fasihi unafaa kufundishia historia. Hivyo basi, hoja mbalimbali zinabainishwa ili kuonesha namna ambavyo riwaya ya Kiswahili ilivyo na nafasi ya kutumika kufundishia historia. Katika makala haya, tumeepuka kujiegemeza katika riwaya za kihistoria zilizozoeleka tu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kuna riwaya nyingi ambazo hazichukuliwi kuwa ni za kihistoria lakini zina mengi ya kutueleza kuhusu historia kama inavyobainishwa katika makala haya. Pia, makala haya yametalii hali ilivyo hivi sasa hususan katika kuangalia namna riwaya zinavyotumiwa na baadhi ya wataalamu wa uga wa historia kufundishia mada mbalimbali za historia. Makala yanabainisha pia namna mbili za ufundishaji wa historia kupitia riwaya; Namna ya kwanza ni kuhusu maarifa ya jumla kuhusu uwanja wa historia yanavyojitokeza katika riwaya. Namna ya pili ni kuhusu ufundishaji wa dhana za falsafa ya historia kupitia riwaya. Pia, makala haya yameonesha changamoto zilizopo katika kuitumia riwaya kufundishia historia na pia yanaibua hatua mwafaka za kuondokana na changamoto hizo. Kwa hakika tunayatazama makala haya kama msaada mkubwa katika kuuangaza uhusiano wa muda mrefu sana kati ya riwaya na historia na namna ya kuutumia uhusiano huo kuihalalisha riwaya ya Kiswahili itumike kufundishia historia.