Main Article Content

Tafsiri Sisisi na Athari zake katika Mawasiliano


OJ Omari

Abstract

Lugha ni chombo muhimu cha mawasiliano katika jamii. Katika mawasiliano andishi, matumizi ya lugha hustahili kuwa wazi na yasiyokanganya kwa kuwa mwandishi hana fursa ya kuufafanua ujumbe nuiwa kama vile inavyotokea katika mawasiliano zungumzi. Suala la athari ya lugha ya kwanza katika ujifunzaji lugha ya pili limewavutia watafiti wengi kote ulimwenguni. Makala haya yanajikita katika suala la tafsiri sisisi kutoka lugha mama na athari yake katika mawasiliano ya Kiswahili. Data ya makala haya inatokana na insha 100 zilizoandikwa na wanafunzi wa shule za upili wilayani Nakuru, Kenya. Ukusanyaji wa data ulifanywa katika shule 10 teule katika wilaya hiyo. Insha zilizoandikwa na wanafunzi hao zilichanganuliwa huku makosa yakibainishwa na kuainishwa kwa kina. Makosa yaliyotokana na tafsiri sisisi kutoka lugha mbalimbali za kwanza pamoja na Kiingereza yamechanganuliwa huku athari zake katika uwasilishaji wa ujumbe ikiwekwa wazi. Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa lugha inayotumiwa na watafitiwa kutoka jamii-lugha mbalimbali iliathiri lugha lengwa (Kiswahili) kutokana na kuhamishwa kwa miundo na maumbo kutoka lugha za kwanza hadi lugha ya pili kwa njia isiyokubalika. Vipengele vilivyoathiriwa zaidi na hali hii ni maneno, sehemu za tungo, na hata tungo nzima. Uchanganuzi huu wa makosa yatokanayo na tafsiri sisisi utawasaidia walimu, wanafunzi, waandishi wa vitabu vya Kiswahili, na wakuza mitaala katika kutengeneza mikakati ya kuwawezesha kupunguza utokeaji wa makosa katika mawasiliano.

Journal Identifiers


eISSN: 0856-552X
print ISSN: 0856-552X