Main Article Content

KISWAHILI AU KIINGEREZA? SIASA NA LUGHA MUAFAKA YA KUFUNDISHIA TANZANIA


B.F.Y.P Masele

Abstract

Madhumuni ya makala hii ni kuonyesha kuwa wataalam wenye wajibu wa kushughulikia tatizo la utayari wa Kiswahili katika elimu walishamaliza kazi yao zamani na wakabainisha kuwa, kwa Tanzania, Kiswahili kikitumika mara moja katika mfumo mzima wa elimu badala ya Kiingereza au lugha nyingine, mabadiliko ya kweli katika maisha ya Mtanzania yataonekana. Kwa kujumuisha mahitimisho ya makala za wataalam mbalimbali, makala hii imetumia nadharia ya udenguzi (Njogu na Chimerah 1999) kuonyesha kuwa lugha ya kuwafundishia Watanzania maarifa ya kuyadhibiti mazingira yao makuu ya ndani ya Tanzania na kuyaishi ilishajulikana tangu zamani. Tatizo ni utekelezaji wake tu. Nadharia hii inaweza pia kuitwa ya kuumbua, au kusambaratisha undani wa dhana iliyoumbwa, kama ilivyojadiliwa na mwaasisi wake, Derrida (1967, 1981), na kuendelezwa na wengine. Kuumbua ni nadharia inayotumika kuweka bayana vitu ambavyo havisemwi, aidha kwa kusema vichache tu au kwa kutukuza dhana moja na kuziua nyingine, na kwa hiyo kuacha mashimo wazi na mapengo ya mantiki. Mashimo haya hutumbukiza watu katika shimo la imani, wakastarehe, wakadhani wamefika ndani ya kiini cha matatizo, kumbe kuna viini vingine vimefichwa makusudi na watoa hoja. Makala hii pia inatoa mapendekezo ya utatuzi wa matatizo kwa kuumbua dhana zenye mapengo, mashimo na utukufu bandia, kwani, mathalani, tatizo la kuendelea kutumia Kiingereza wakati kuna Kiswahili kilicho tayari si tatizo la upungufu wake kitaaluma, kiutafiti au kipedagojia (Mekacha 2000, Mulokozi 2002, Qorro 2003a, 2003b, 2004, Galabawa 2003, 2004; Galabawa na Lwaitama 2004). Mapendekezo hayo ni pamoja na kuidengua chuki waliyonayo wakubwa kwa udenguzi, na kuongeza kwamba, kinachotakiwa sasa ni kuitumia dhana hii ya udenguzi ili kubuni paradaim mpya juu ya matatizo yetu, kama yanavyowakilishwa na tatizo la lugha ya kufundishia Tanzania.

Journal Identifiers


eISSN: 0856-552X
print ISSN: 0856-552X