Main Article Content
Usawiri wa Nduni za Shujaa katika Kisakale cha Munyigumba wa Jamii ya Wahehe
Abstract
Makala hii inachunguza usawiri wa nduni za shujaa katika Kisakale cha Munyigumba wa jamii ya Wahehe. Watafiti wa masuala ya nduni za shujaa wa Kiafrika wanaeleza kuwa kila jamii ina nduni zake za shujaa zinazotegemea mtazamo, falsafa na utamaduni wa jamii husika. Hivyo, si rahisi kwa jamii zisizo na uhusiano wa karibu kuwa na nduni za shujaa zinazolandana katika hali zote. Kuwapo kwa mitazamo na tamaduni tofautitofauti kunasababisha sifa za shujaa wa jamii moja kuwa tofauti na za shujaa anayepatikana katika jamii nyingine. Hivyo, kilichofanyika katika makala hii ni kubainisha nduni za shujaa wa jamii ya Wahehe ili kufahamu nduni zake. Makala hii imeongozwa na mawazo ya Nadharia ya Ontolojia ya Kiafrika kwa kuwa shujaa anayechunguzwa anatoka katika jamii za kijadi za Kiafrika. Data za makala hii zimekusanywa kwa njia ya usaili na uchambuzi matini kutoka katika vijiji vya Kalenga na Rungemba, Mkoani Iringa. Matokeo ya utafiti wa makala hii yameonesha kuwa shujaa wa jamii ya Wahehe ana nduni mbalimbali zilizothibitika kupitia Kisakale cha Munyigumba. Aidha, imethibitika kuwa, jamii mbalimbali za Kiafrika zina mfanano mkubwa unaosababisha hata mashujaa wake kuwa na nduni zinazofanana kwa kiasi kikubwa.