Main Article Content
Dhima ya Nyimbo za Kiswahili za Watoto katika Kujifunza Mazingira
Abstract
Nyimbo ni fani kongwe na ya mwanzo kabisa ya fasihi simulizi kutumiwa na binadamu katika kupambana na mazingira yake. Kwa ujumla, nyimbo ni fani ya fasihi simulizi ambayo hutumika katika hatua na nyanja mbalimbali za maisha ya binadamu. Mojawapo ya vipera vyake ni nyimbo za watoto. Nyimbo hizo, pamoja na mambo mengine, zina hazina kubwa ya mafunzo katika kuyaelewa mazingira ya jamii husika. Mazingira ni kila kitu kinachomzunguka mwanadamu (na mwenyewe akiwamo). Hujumuisha wanadamu, wanyama, mimea, bahari, mawingu, ardhi, majengo, milima na vitu visivyo na uhai. Lengo la makala hii ni kuchunguza mchango wa fasihi ya Kiswahili, hususani nyimbo za watoto, nchini Tanzania katika taaluma ya mazingira. Makala inachunguza namna ambavyo nyimbo za watoto zinatoa maarifa mbalimbali kuhusu mazingira katika kumfunza mtoto na jamii kwa ujumla. Data za utafiti huu zilikusanywa uwandani kwa kusikiliza nyimbo za watoto za Kiswahili kutoka katika muktadha wa kitaaluma na katika mazingira yao wanamoishi. Aidha, data nyingine zilipatikana kwa kupitia maandiko mbalimbali maktabani kuhusu nyimbo hizo. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa nyimbo za Kiswahili za michezo ya watoto ni muhimu kwa watoto na jamii, si tu katika kujifunza mazingira ya jamii mahususi, bali pia katika kuwasilisha maudhui yahusuyo mazingira kwa jamii pana.