Main Article Content
Itikadi za Kisiasa katika Fasihi ya Watoto ya Kiswahili
Abstract
Hadithi katika vitabu vya fasihi ya watoto mara nyingi huwa fupi na vitabu hivyo huwa vidogo mno. Hali hii imechangia waandishi wengi kujiaminisha kwamba watoto wana akili ndogo na hivyo basi ni rahisi mno kuwaandikia vitabu (Fox, 1993). Fox anadai kwamba watoto huwa na uwezo mkubwa wa akili na hali hiyo huchangia katika ugumu wa kuwatungia hadithi. Anasema kwamba ni vigumu zaidi kutunga fasihi ya watoto kuliko fasihi inayolenga hadhira ya watu wazima. Lengo la makala hii ni kuonesha kwamba, humohumo katika usahili unaonuiwa kumnufaisha msomaji mtoto mna uchangamano katika kazi za fasihi ya Kiswahili ya watoto zinaposomwa kwa jicho kali la kiuhakiki kwa misingi ya kinadharia. Makala inakusudia kupambanua namna itikadi za kisiasa zinavyobainika katika fasihi ya watoto kwa kuchambua maudhui katika tungo hizo. Tungo zinazohakikiwa ni: Usininyonye (Komora, 1971), Mkasa wa Shujaa Liyongo (Matundura, 2001), Karamu Mbinguni (Kimunyi, 2002), Zimwi la Leo! (Wamitila, 2002) na Sungura Mpanda Ngazi (Kobia, 2008). Usampulishaji wa kimakusudi umetumika kuteua kazi hizi. Usomaji wa matini umeegemezwa katika Nadharia ya Umaksi. Je, tunaweza kupata fasiri tofauti inayohusiana na siasa mbali na ile wanayopata watoto wanapozisoma tungo hizi bila kutumia nadharia? Majibu ya swali hili yanapatikana katika makala hii.