Main Article Content
Ruwaza ya Utatu wa Sinonimu za Asili na za Mkopo katika Kiswahili
Abstract
Ukopaji wa maneno katika lugha husababisha lugha pokezi kuwa na msamiati changamani, yaani msamiati wa asili na wa mkopo (Kiango, 1999). Inasemekana kuwa lugha inapokuwa na maneno ya asili na ya mkopo hutokea wakati neno la asili likawa na uhusiano wa kimaana na neno moja au zaidi kutoka lugha za kigeni moja au zaidi na, hivyo, kuibua sinonimu zinazohusisha maneno ya asili na ya mkopo. Ullmann (1967) anaeleza kuwa visawe vya dhana moja katika lugha kutoka lugha mbalimbali havijakaa kivoloya, bali hufuata ruwaza fulani. Ruwaza hizo huitwa ruwaza za sinonimu. Ruwaza hizo zinaweza kuwa za uwili au utatu (Ullmann, 1967; Kreidler, 1998). Lugha ya Kiswahili imedhihirisha sifa ya kuwa na msamiati changamani kwa sababu ya kutohoa maneno mengi kutoka lugha za kigeni. Kuwapo kwa msamiati changamani katika lugha hii hapana shaka kuna sinonimu zinazojitokeza ambazo zinatengeneza ruwaza mbalimbali. Makala hii inachunguza ruwaza ya utatu wa sinonimu za asili na za mkopo katika Kiswahili. Data za makala hii zimekusanywa kutoka Kamusi ya Kiswahili Sanifu (KKS) (2013), Kamusi ya Visawe (KV) (2014) na Kamusi Kuu ya Kiswahili (KKK) (2017) pamoja na kutoka kwa watoataarifa. Data kutoka vyanzo hivyo zimekusanywa kwa kutumia mbinu za uchambuzi wa matini, usaili na hojaji na kuchambuliwa kwa kutumia mbinu ya uchambuzi wa data kimaudhui na kiulinganishi. Mjadala wa makala hii umeongozwa na nadharia mbili: Nadharia ya Vijenzi pamoja na Nadharia ya Matumizi.