Main Article Content

Ufasihi wa Matambiko: Uchunguzi wa Matambiko ya Wapangwa


Winne Stephen Mtega

Abstract

Mojawapo ya sifa msingi zinazoipambanua fasihi ni matumizi ya lugha ya kisanaa (Mulokozi, 2017). Dhana ya ufasihi hujengwa kutokana na matumizi ya lugha teule, yenye ubunifu ndani yake na ambayo huweza kuvuta hisia za wasomaji au wasikilizaji wa kazi husika. Mpaka sasa kumekuwa na mjadala baina ya wanazuoni hususani wa fasihi kuhusu ufasihi wa tambiko. Mjadala huo umeibuka kwa lengo la kuhoji juu ya ufasihi uliopo kwenye tambiko na hata kudadisi ikiwa tambiko ni kipera cha fasihi au la (Samwel, 2013, 2015; Mulokozi, 2017). Samwel (2013) anatoa mtazamo wake kwa kueleza kuwa kinachochukuliwa kuwa ni fasihi katika tambiko ni maneno, yaani lugha ya kisanaa iliyotumika, manuizo pamoja na nyimbo na si matendo matupu yasiyo na maneno. Ufafanuzi wake ni muhimu japo hautoi ithibati yoyote inayoonesha udhihirikaji wa ufasihi huo. Kutokana na jambo hili kutokuwa wazi, makala hii imechunguza ufasihi wa tambiko na mifano imetolewa kutoka katika matambiko ya Wapangwa. Katika kufanikisha hilo, Nadharia ya Utendaji imetumika huku mawazo yake makuu yakisaidia kubainisha viashiria mbalimbali vya kifasihi vilivyojitokeza katika utendaji wa tambiko. Data za mjadala huu zilipatikana uwandani kupitia njia ya mahojiano na majadiliano ya kwenye vikundi ambayo yalifanyika baada ya kumaliza tukio la utambikaji. Makala hii ilibaini vipengele kadhaa vya kifasihi vilivyojitokeza katika matambiko ya Wapangwa. Baadhi ya vipengele hivyo ni matumizi ya mbinu za kishairi, takriri, tabano, nyimbo na lugha ya picha. Ujitokezaji wa vipengele hivyo vya kifasihi unadhihirisha ufasihi uliopo katika matambiko na kuyafanya yakidhi kuwa moja ya kipera cha fasihi simulizi.


Journal Identifiers


eISSN: 0856-552X
print ISSN: 0856-552X