Main Article Content
Euphrase Kezilahabi: Jabali katika Utetezi wa Uafrika
Abstract
Jina Euphrase Kezilahabi si geni katika ulimwengu wa fasihi. Umahiri katika uandishi wa kazi zake za fasihi, umezua mijadala mingi katika uga wa taaluma. Kimsingi, mijadala hiyo inabainisha mchango wake katika maendeleo ya fasihi, kwa namna kazi zake zinavyojipambanua kifani na kimaudhui. Hata hivyo, pamoja na mijadala ya wataalamu hao kuutajirisha uga wa kitaaluma kwa kujadili mchango wa nguli huyo katika maendeleo ya fasihi, bado suala la namna Kezilahabi anavyojipambanua katika kuutetea Uafrika, halijatazamwa kwa kina. Makala hii inaziba pengo hilo la kitaaluma kwa kubainisha namna mwandishi huyo alivyojipambanua katika kuutetea Uafrika, mahususi katika mwegamo wa kitamaduni. Data zilizozalisha makala hii zilikusanywa maktabani na uwandani. Data za msingi zilikusanywa kutoka katika riwaya teule za Dunia Uwanja wa Fujo, Nagona, na diwani ya Karibu Ndani. Data hizi zilipewa ithibati na data za upili zinazohusiana na mada husika ambazo zilikusanywa uwandani na maktabani. Uchanganuzi na uwasilishaji wa data ulifanyika kwa kutumia Nadharia ya Sosholojia ya Fasihi. Makala imebainisha namna Euphrase Kezilahabi anavyojipambanua katika kuutetea Uafrika kupitia maisha yake halisi na katika kazi zake za fasihi.