Main Article Content
Jaala za Mashujaa Zinazojitokeza katika Tendi za Nanga
Abstract
Makala hii imechunguza jaala za mashujaa zinazojitokeza katika tendi za Nanga. Tendi hizo ni Rukiza, Mugasha na Kachwenyanja. Lengo la makala hii ni kuweka bayana jaala za hatima zilizopo katika tendi za Nanga kulingana na ontolojia ya jamii za Kiafrika. Data za makala hii zilikusanywa kutoka uwandani na maktabani. Mbinu za uchanganuzi wa matini na mahojiano zimetumika katika ukusanyaji wa data. Uchambuzi wa data umeongozwa na Nadharia ya Ontolojia ya Kiafrika. Matokeo ya utafiti katika tendi hizo yanaonesha kuwa mashujaa wa tendi za Nanga wanafungamana na jaala mbili za hatima. Jaala ya shujaa iliyojitokeza katika utendi wa Rukiza ni jaala ya ustawi wa jamii ya Baganga na jaala ya utawala. Katika utendi wa Mugasha kuna jaala ya bahati ya kuoa mwanamke na jaala ya utawala. Kwa upande wa utendi wa Kachwenyanja kuna jaala ya kutafsiri ndoto ambayo imeundwa na jaala ya bahati ya kuoa mwanamke na jaala ya kifo. Aidha, katika tendi za Nanga shujaa akifungamana vizuri na jamii yake kupitia vipengele mbalimbali vya kiontolojia anafanikiwa kutimiza jaala yake. Vilevile, shujaa akivunja mshikamano kati yake na ontolojia ya jamii yake anashindwa kutimiza jaala yake.