Main Article Content
Uenezi wa Kiswahili baada ya Uhuru wa Afrika Mashariki kwa Mtazamo wa Nadharia ya Mifumo Changamano
Abstract
Kiswahili ni lugha pekee ya Kiafrika ambayo imejinyakulia nafasi ya juu miongoni mwa lugha za kimataifa. Imefikia umataifa huu kutokana na kuenea kwake kijiografia na kimatumizi ndani na nje ya Afrika Mashariki, eneo ambalo ni kitovu chake cha pili hasa cha Kiswahili Sanifu ambayo ni lahaja inayokuzwa kimataifa. Kitovu chake cha kwanza hasa kwa lahaja zake asilia kikiwa mwambao mwa Afrika. Uenezi huu umekuwa wa kasi baada ya nchi za Afrika Mashariki - Tanzania, Uganda na Kenya - kupata uhuru mwanzoni mwa miaka ya 1960. Uhuru huu ulifanya Kiswahili kuenea katika eneo hili hadi kujitwalia hadhi ya kuwa lingua franka. Nchi hizi huru ziliinua hadhi ya Kiswahili kwa njia tofauti; Tanzania iliifanya lugha rasmi, Kenya lugha ya taifa, na Uganda lugha rasmi kwa amri ya Rais mnamo mwaka 1973 (Pawlikova-Vilhanova, 1996). Japo amri hii ya Rais haijatekekezwa hadi sasa, Kiswahili bado kinatumika nchini Uganda kama lugha ya jeshi na polisi na kama lingua franka katika mitagusano ya kibiashara na kijamii. Hadhi hii imesaidia kuenezea Kiswahili ndani na nje ya Afrika. Japo uenezi huu una motisha, haibainiki wazi jinsi shughuli za ujenzi wa mataifa haya zilivyokuza uenezi wake hadi kuufikisha kiwango cha kimataifa katika miongo mitano pekee ikizingatiwa kuwa, si nchi zote zilizoweka mikakati ya kuikuza. Kwa kuwa uenezi wake umefungamana na shughuli za kimaendeleo katika mataifa haya, makala hii imechunguza uenezi wake kwa mtazamo wa Nadharia ya Mifumo Changamano.