Main Article Content
Mchango wa Mradi wa Vitabu vya Watoto katika Kuikuza na Kuiendeleza Fasihi ya Watoto Tanzania
Abstract
Fasihi ya watoto nchini Tanzania, kama taaluma, ilianza katika mazingira ambayo si rasmi sana. Kwa kiasi kikubwa uandishi wa vitabu vya fasihi ya watoto ulichipuka kama juhudi za kuinua na kujenga mazoea na tabia ya usomaji miongoni mwa watoto chini ya Mradi wa Vitabu vya Watoto (Madumulla, 2001; Traore, 2011). Ipo mikondo miwili ya historia ya Mradi wa Vitabu vya Watoto Tanzania ambayo inaonesha kwamba malengo ya Mradi yalikuwa na mielekeo miwili tofauti lakini inayoishia katika mwisho unaofanana. Mikondo hiyo miwili kuhusu asili ya Mradi imejadiliwa katika makala hii. Hata hivyo, pamoja na mjadala wa mikondo hiyo, kwa kiasi kikubwa, makala hii imejikita katika kujadili mchango wa Mradi katika kukuza na kuendeleza fasihi ya watoto Tanzania. Historia ya taaluma ya fasihi ya Kiswahili ya watoto nchini Tanzania inahusishwa zaidi na Mradi wa Vitabu vya Watoto Tanzania pamoja na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI). Pamoja na maendeleo ya fasihi ya watoto kuhusishwa zaidi na taasisi hizo mbili, makala hii itajikita katika kujadili mchango wa Mradi wa Vitabu vya Watoto katika kukuza uwanja wa fasihi ya watoto Tanzania.