Main Article Content

Mapokezi ya Kisemantiki ya Nomino za Mkopo katika Kiswahili: Mifano kutoka Nomino zenye Asili ya Kiingereza na Kiarabu


Musa Mohamed Salim Shembilu

Abstract

Nomino za mkopo zinapoingia katika lugha kopaji huwa zinachakatwa katika viwango mbalimbali vya kiisimu. Nomino hizo zinaweza kuchakatwa katika kiwango cha kifonolojia, kimofolojia au kisemantiki. Michakato hiyo hutokea wakati wa kuzipokea nomino hizo ili kuzifanya ziendane na mfumo wa lugha kopaji. Lengo la makala hii ni kuchunguza namna nomino za mkopo zinavyopokewa kisemantiki katika Kiswahili. Je, nomino hizo zimepokewa na maana zake zote kama zilivyo katika lugha kopwaji au zimefanyiwa marekebisho yoyote? Kama zimefanyiwa marekebisho wakati wa kupokewa katika Kiswahili ni marekebisho gani hayo? Je, maana za nomino hizo zimepanuliwa, zimepunguzwa au zimegeuzwa? Vilevile, makala hii inachunguza sababu za mabadiliko ya maana zinazojitokeza wakati wa kupokewa kwa nomino za mkopo katika Kiswahili. Makala hii inaongozwa na Nadharia ya Sarufi Amilifu (Functional Grammar Theory) inayosisitiza kuwa mabadiliko ya maana ya maneno huukiliwa na matumizi ya maneno hayo na mahitaji ya mawasiliano ya jamii. Hivyo, mabadiliko ya maana yaliyotokea katika nomino za mkopo katika Kiswahili yanatokana na namna jamii ya Waswahili1 wanavyozitumia nomino hizo au kutokana na mahitaji yao ya kimawasiliano. Makala hii inatarajiwa kuwa na manufaa katika taaluma ya semantiki kwa kuweka bayana namna nomino zinavyochakatwa kisemantiki na sababu ya kuchakatwa huko.

Journal Identifiers


eISSN: 0856-552X
print ISSN: 0856-552X