Main Article Content
Uhifadhi na Upanuzi wa Wigo wa Matumizi wa Lugha ya Kiswahili nchini Tanzania
Abstract
Lengo la makala haya ni kujadili mbinu mbalimbali zinazoweza kutumika ili kuihifadhi lugha ya Kiswahili. Mara nyingi uhifadhi wa lugha umekuwa ukihusishwa na lugha zisizokuwa na wazungumzaji wengi, ambazo hadhi yake ni duni kimatumizi ikilinganishwa na lugha zinazotumika kwa mawasilino mapana kama lugha za taifa. Dhana hii huhusishwa na lugha ambazo ziko hatarini kutoweka (Salikoko, 2004). Nchini Tanzania lugha hizo ni zile za makabila. Hata hivyo, katika makala haya tunaangalia uhifadhi wa lugha kubwa yenye majukumu makubwa kitaifa kama lugha kuu ya mawasiliano. Lugha hii ni Kiswahili. Kwa mujibu wa ripoti ya jopo la wataalamu wa UNESCO (2003) lugha yoyote ile inaweza kupata misukosuko na ikaathirika kutokana na nguvu za kiuchumi, kivita, kidini au ugandamizwaji kielimu. Pia lugha inaweza kuathirika kutokana na mtazamo hasi wa watumiaji wa lugha. Lugha kubwa pia zinaathirika kutokana na nguvu za utandawazi unaotukuza lugha za kigeni. Lugha ya Kiswahili ni amali muhimu kwa mawasiliano na kitambulisho cha jamii yake kama ilivyo lugha yoyote ya jamii fulani, hivyo basi uhifadhi wa lugha hii ni muhimu ili iweze kudumu na kurithishwa kwa vizazi vijavyo. Katika makala haya tunajadili njia mbalimbali za uhifadhi wa lugha ya Kiswahili na changamoto zinazowakabili wataalamu wa lugha.