Main Article Content
Majuto ni Mjukuu: Uchunguzi wa Mhusika Ngoma katika Riwaya ya Ua la Faraja
Abstract
Maisha ya mtu ni hadithi inayopaswa kusimuliwa ili kutoa mafunzo kwa jamii kuhusu mapito ya mhusika. Hii inatokana na ukweli kwamba kila mtu katika jamii ana mambo mazuri na/au mabaya ya kusimulia yanayohusu mapito ya maisha yake. Yapo masimulizi yanayofurahisha kutokana na matendo ya mhusika na mengine husikitisha kiasi cha kumfanya mhusika kuyajutia maisha yake kutokana na kufanya au kutofanya jambo fulani. Kwa msingi huo, makala hii ililenga kuchunguza methali inayosema “majuto ni mjukuu” kwa kuchunguza maisha ya mhusika Ngoma katika riwaya ya Ua la Faraja (2004). Mhusika huyu ameteuliwa kama kiwakilishi cha wahusika wengi ambao katika maisha yao, walifanya na/au hawakufanya mambo fulani ambapo kutokana na kufanya na/au kutokufanya kwao, kulisababisha majuto katika maisha yao. Pia, riwaya hii imeteuliwa kama sampuli ya riwaya mbalimbali zenye wahusika wenye sifa kama za mhusika Ngoma. Data zilitokana na uchambuzi wa riwaya ya Ua la Faraja. Vilevile, Nadharia ya Uhalisia ilitumika kama mwongozo katika ukusanyaji wa data, uchambuzi na uwasilishaji wa matokeo ya utafiti wa makala hii. Matokeo yanaonesha kwamba ziko sababu kuu nne zilizosababisha Ngoma ayajutie maisha yake. Sababu hizo ni kukosa uaminifu katika ndoa, kuitelekeza familia yake, kuendekeza anasa, na kutowajali ndugu zake.