Main Article Content
Epistemolojia ya Waafrika katika Semi Zilizoandikwa kwenye Vazi la Kanga za Waswahili
Abstract
Epistemolojia ya Waafrika, wakiwamo Waswahili hubainika kupitia sanaa inayobeba mitazamo inayozingatiwa katika jamii yao. Moja kati ya mambo yanayobainisha sanaa ya Waswahili ni vazi la kanga. Kwa jumla, usanaa katika vazi hilo hudhihirika kupitia maumbo au michoro na lugha ya kiufundi ambayo hubeba semi kama vile, mafumbo, methali na misemo. Vazi la kanga huthaminiwa na hutumiwa kwa namna mbalimbali katika maisha ya Waswahili, mathalani, kufunga kiunoni, kichwani, kujifunika na kama pambo (Hanby na Bygott, 1984). Kwa jumla, semi zilizoandikwa kwenye vazi la kanga zimefafanuliwa zaidi katika muktadha wa dhamira na dhima pasipo kumakinikiwa kwa kina katika muktadha wa kiepistemolojia kulingana na kaida za Waswahili wenyewe. Makala haya yanafafanua namna semi hizo zinavyobeba na kuhifadhi maarifa ya kiepistemolojia yanayosawiri maisha halisi ya Waswahili. Vilevile, misingi ya Nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi imetumika kama mwegamo mkuu katika kuchunguza, kuchanganua na kuwasilisha data husika. Matokeo yanaonesha kuwa maandishi yaliyopo katika vazi la kanga yanahifadhi fasihi ya Waswahili, hususani semi ambazo hubainisha maarifa mbalimbali, yakiwemo ya kiepistemolojia. Hivyo, makala haya yanajadili baadhi ya vipengele hivyo ambavyo ni: maarifa kuhusu kuwapo kwa kani kuu, thamani ya kazi, heshima na utiifu na uvumilivu.