Main Article Content

Tathmini ya Matumizi ya Akili Unde Kama Nyenzo ya Kutafsiri Matini za Kiingereza Kwenda Kiswahili


Hadija Jilala

Abstract

Dhana ya akili unde au akili bandia inarejelea mwigo au ukadiriaji wa akili ya binadamu katika mashine. Lengo la akili unde ni pamoja na  matumizi ya kompyuta yaliyoboreshwa kuhoji na kutambua mambo anuwai unde na ya tasnia mbalimbali (Jurafsky na Martin, 2020).  Makala hii inalenga kutathmini matumizi ya akili unde kama nyenzo ya kutafsiri matini za Kiingereza kwenda Kiswahili. Data ya makala hii imekusanywa maktabani kwa kupitia maandiko na pia uwandani kwa kuwahoji wanataaluma mbalimbali. Uchambuzi na uwasilishaji wa  data ya makala hii umeongozwa na Mkabala wa Uchambuzi wa Maudhui ya Krippendorff (2004). Matokeo ya uchunguzi yanaonesha  kuwa akili unde ina ubora kwa vile hufanya kazi kwa kasi, gharama ni nafuu, urahisi, kutafsiri lugha nyingi na unyumbufu wa  kuunganishwa na teknolojia nyingine. Kwa upande mwingine makala hii imebainisha udhaifu wa matumizi ya akili unde kama vile  kutozingatia muktadha, kukosa ubunifu, tofauti za kiisimu, kukosa usalama na upinzani wa wanaisimu. Kutokana na udhaifu huo, Makala hii inapendekeza kuwa uwekwe uangalizi wa binadamu katika mifumo, kushughulikia utata, kuboresha mifumo kila muda, kuwekwe  sehemu ya maoni ya mtumiaji na matumizi ya mbinu msetu. Hivyo, ni muhimu kuweka usawa kati ya ufanisi wa mashine na uelewa wa  watafsiri wa kibinadamu katika uendelezaji na utekelezaji wa akili unde katika tafsiri.   


Journal Identifiers


eISSN: 2958-4914