Main Article Content
Mtazamo wa Ki-Afrika katika Nadharia za Tafsiri
Abstract
Makala haya yanahusu Mtazamo wa Ki-Afrika katika Nadharia za Tafsiri. Inafahamika kuwa chimbuko la nadharia za tafsiri zilizopo ni nchi za Kimagharibi. Hata hivyo, katika nchi za Afrika taaluma ya tafsiri imepiga hatua kubwa ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuwa na wataalamu na wanataaluma wengi wa tafsiri, kufundishwa katika shule za sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu. Pamoja na maendeleo hayo, mpaka sasa hakuna nadharia ya tafsiri iliyobuliwa kupitia mazingira, muktadha na utamaduni wa lugha ya Kiswahili kama lugha ya Ki-Afrika. Hivyo, makala haya yanalenga kujadili umuhimu wa kuunda nadharia za tafsiri kwa kutumia muktadha wa lugha za Ki-Afrika na kupendekeza hatua zitakazochukuliwa katika mchakato wa kuunda nadharia za tafsiri za Kiswahili. Makala yanajadili kwamba, pamoja na kuwapo kwa nadharia zilizoibuliwa na wanazuoni wa Kimagharibi, kuna umuhimu wa kuunda nadharia za tafsiri ambazo zimefungamana na muktadha, mazingira, mila, desturi, historia, lugha na utamaduni wa Ki-Afrika. Hii ni kwa sababu tafsiri hushughulika na lugha ambayo ni mali ya jamii yenye utamaduni mahususi. Hivyo, nadharia za tafsiri zilizofumbata mtazamo wa Ki-Afrika zitakuwa msingi, dira na mwongozo wa kinadharia na kivitendo katika kushughulikia tafsiri za matini mbalimbali za lugha za Ki-Afrika, hasa zinazohusu dhana za kiutamaduni na fasihi. Vilevile nadharia hizo zitakuwa ni suluhisho la matatizo na changamoto za tafsiri kiisimu, kisemantiki, kiutamaduni na kifasihi. Makala haya yanapendekeza kuwa nadharia za tafsiri zinaweza kuundwa kwa kutumia mbinu mbalimbali kama vile kuunda nadharia mpya, kuasili nadharia zilizopo na kuziboresha nadharia hizo.