Main Article Content
Tafsiri au uandishi mpya: Uchambuzi wa tamthiliya ya Kinjeketile
Abstract
Tafsiri hujishughulisha na usafirishaji wa ujumbe ulio katika maandishi kutoka lugha asilia kwenda lugha pokezi ambao hufanywa na mwandishi mwenyewe au mtaalamu mwingine. Makala haya yanachunguza tamthiliya ya Kinjeketile iliyoandikwa kwa Kiswahili kwa mara ya kwanza mwaka 1969 kisha ikatafsiriwa kwa Kiingereza na mwandishi mwenyewe Ebrahimu Hussen kama Kinjeketile mwaka huo huo wa 1969. Kimahususi, makala inachunguza ni kwa namna gani mtafsiri ameweza kuweka usawa wa ujumbe na mtindo baina ya matini asilia na matini pokezi wakati yeye ndiye mwandishi wa tamthiliya hiyo na ameitafsiri mwaka huo huo. Je alitafsiri au aliandika tamthiliya mpya iliyo katika lugha ya Kiingereza? Utafiti umetumia mkabala wa kistahilifu linganishi (correlation qualitative design) kwa kiasi kikubwa japo mkabala wa takwimu umejitokeza kidogo. Data zimekusanywa kwa kutumia mbinu ya upekuzi matini (documentary review). Nadharia ya ulinganifu imetumika katika uchanganuzi wa data kama ilivyojadiliwa na Nida (1964), Catford (1965) na Newmark (1988). Utafiti umebaini kuwa tamthiliya ya Kinjeketile ya Kiingereza ni matini mpya na sio tafsiri kutokana na utofauti wake katika utangulizi, muundo pamoja na idadi na utumizi wa majina ya wahusika.