Main Article Content

Hali ya lugha ya Kiswahili katika vyuo vikuu nchini Tanzania: Mifano kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere


Sauda Uba Juma
Editha Adolph

Abstract

Watafiti wa makaka hii wanaangazia hali ya lugha ya Kiswahili katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA1 kuanzia sasa). Azma ya uchunguzi huo ni kutaka kubaini endapo lugha ya Kiswahili inapewa nafasi stahiki katika Chuo hicho au la. Hii inatokana na ukweli kwamba kuna baadhi ya taasisi ambazo zinaithamini sana lugha ya Kiswahili na kuipa nafasi sawa na lugha nyingine za kigeni. Hata hivyo, zipo baadhi ya taasisi ambazo zinaibeza lugha hii na kuiona kama kwamba haina nafasi yoyote kitaaluma na kimawasiliano. Data ya makala hii imekusanywa kupitia njia tatu: upitiaji wa nyaraka mbalimbali kutoka maktabani, usaili na ushuhudiaji. Hivyo, njia zote hizo kwa pamoja zimetusaidia kupata data faafu na ya kutosha kulingana na malengo ya makala hii. Vilevile, uchambuzi wa data katika utafiti huu, umetumia mkabala wa kitaamuli ambapo mbinu za kimaelezo na kiufafanuzi zimetumika katika kudadavua vipengele mbalimbali ambavyo vimebainishwa. Sanjari na mkabala huo, tumetumia pia mkabala wa kitakwimu ambao kimsingi umejikita katika uchambuzi wa data kwa kutumia namba. Mkabala huu ulitumika pale tu ilipobidi kufanya hivyo ili kuonesha idadi ya baadhi ya vipengele vilivyokuwa na uhitaji huo. Aidha, matokeo yameonesha kwamba, kuna mabadiliko na mafanikio makubwa MNMA katika kuikuza na kuiendeleza lugha ya Kiswahili, tofauti na ilivyokuwa hapo awali. Tunadiriki kusema hivyo kwa kuwa tumebaini juhudi lukuki za makusudi zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa kwa minajili ya kuikuza na kuiendeleza lugha hii ya Kiswahili.


Journal Identifiers


eISSN: 2958-4914
 
empty cookie