Main Article Content

Ujitokezaji wa viarudhi vya kifonolojia katika Kihaya: uchunguzi kifani wa toni katika lahaja ya Kihamba


Editha Adolph

Abstract

Fonolojia ni taaluma iliyosheheni viarudhi au vipambasauti kama ambavyo wataalamu wengine huviita. Miongoni mwake ni toni, lafudhi, mkazo, nguvumsikiko, usilabi, kiimbo, unguvunguvu, kidatu na wakaa. Viarudhi hivi hupatikana takribani katika kila lugha ingawaje baadhi ya lugha huwa navyo vichache na kukosa baadhi. Toni ni miongoni mwa viarudhi vinavyojitokeza katika Kihaya. Makala hii inachunguza jinsi kiarudhi hiki kinavyojitokeza katika Kihaya hususan lahaja ya Kihamba na namna ambavyo huathiri maana ya msamiati sambamba na kubadili kategoria katika lahaja hiyo. Lahaja ya Kihamba ni miongoni mwa lahaja za Kihaya. Lahaja nyinginezo za lugha hii ni: Kinyaihangiro, Kinyambo na Kiziba. Data ya makala hii imekusanywa uwandani kwa kushuhudia mazungumzo mbalimbali ya wazungumzaji wa lahaja ya Kihamba katika nyakati tofautitofauti na sehemu mbalimbali, pia mbinu ya usaili kutoka kwa wazungumzaji wa lahaja hii ilitumika. Ulifanyika pia uchambuzi wa matini mbalimbali kutoka maktabani mathalani, kamusi, majarida, tasinifu, tafiti na nyaraka mbalimbali zinazohusiana na mada inayoshughulikiwa katika makala hii. Kwa kutumia mbinu ya usaili, nomino na vitenzi mbalimbali viliandaliwa kwa Kiswahili na watoa taarifa walihitajika kuvitamka kwa Kihaya hususani Kihamba huku mtafiti akirekodi na kualamisha toni katika nomino na vitenzi hivyo. Data imechanganuliwa kwa kutumia mkabala wa maelezo. Nadharia iliyotumika kuchanganua data ya makala hii ni Nadharia ya Fonolojia Vipandesauti Huru iliyoasisiwa na Goldsmith (1976). Matokeo ya makala hii yanaonesha kuwa toni hujitokeza katika Kihaya hususani lahaja ya Kihamba. Imebainika pia kuwa toni hizi zimesheheni uamilifu wa kubadili maana na kategoria za msamiati kutokana na tofauti za kimatamshi zinazosababishwa na matumizi ya toni ya juu au ya chini katika msamiati wenye kufanana kiothografia. Aidha, matokeo yanaonesha kuwa si kila kitenzi au nomino hutamkwa kwa namna tofauti kutokana na kutokubali kupokea toni juu J (kuanzia sasa) na wakati huohuo toni chini C (kuanzia sasa). Aidha, makala hii imetoa ufafanuzi na kuonesha uamilifu wa toni katika lahaja ya Kihamba na hivyo kuwapa mwanga wanaisimu juu ya kiarudhi hiki cha kifonolojia. Inapendekezwa kuwa viarudhi vingine mathalani lafudhi, mkazo, nguvumsikiko, usilabi, kiimbo, unguvunguvu, kidatu na wakaa vifanyiwe uchunguzi katika Kihaya na lugha nyinginezo. Pia lichunguzwe suala la ujitokezaji wa toni katika aina nyingine za maneno katika lugha hii tofauti na nomino na vitenzi. Kwa mfano, vielezi, vivumishi, vihisishi na kadhalika. Aidha, tafiti fuatizi zaweza kuangazia matumizi ya toni katika lugha za Kiafrika.


Journal Identifiers


eISSN: 2958-4914