Main Article Content
Makosa yanayofanywa na wanafunzi katika ujifunzaji wa isimu: mifano kutoka chuo cha kumbukumbu ya mwalimu nyerere
Abstract
Makala haya yanachunguza na kutathmini makosa yanayofanywa na wanafunzi katika mchakato mzima wa ufundishaji na ujifunzaji wa kozi mbalimbali za kiisimu kwa wanafunzi MNMA. Mchakato huo uliangaza wanafunzi wanaosoma kozi za isimu ya Kiswahili darasani. Lengo la kuona haja ya uchunguzi huo, ni kubaini makosa mbalimbali yanayofanywa na wanafunzi hao na kutafuta njia mbadala ya kuweza kuwasaidia. Data za makala haya zilikusanywa kwa njia nne ambazo ni: Mosi, udurusu wa nyaraka mbalimbali maktabani ili kuwa na welewa mpana zaidi unaohusu vipengele anuwai vya kiisimu vilivyochunguzwa. Pili, hojaji ambazo zilihusisha vipengele mbalimbali vya kiismu kama vile fonolojia, mofolojia, sintaksia na semantiki zilitumika kwa ajili ya kupata data na kubaini makosa ya kiisimu yaliyojitokeza. Tatu, usaili ambapo baadhi ya wanafunzi waliochaguliwa kinasibu, walitakiwa kutoa maoni yao na kujadiliana na mtafiti kuhusu vipengele hivyo. Mwisho, njia ya ushuhudiaji ilitumika wakati wa mijadala iliyoendeshwa darasani katika vipindi vyao kulingana na ratiba iliyowekwa. Njia hii ilitusaidia kupata data za kiisimu kupitia utamkaji na uzungumzaji. Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba kuna matatizo kadhaa ambayo yanawakwama wanafunzi na kusababisha kufanya makosa na kuona ugumu katika kujifunza isimu ya Kiswahili. Hivyo, makosa hayo yaliyofanywa yamebainishwa na kupendekeza namna bora ya kuwasaidia vijana hao ili baadhi yao wasiendelee kuzichukia baadhi ya kozi za kiisimu kama vile fonoloji, mofoloji, sintaksia na semantiki