Main Article Content
Uamilifu wa Ngazi ya Utambuzi katika Riwaya Teule za Kiswahili
Abstract
Makala haya yanachunguza ngazi ya utambuzi na uamilifu wake katika riwaya za Kiswahili zilizoteuliwa makusudi kwa uchunguzi huu. Riwaya hizo ni; Nyuso za Mwanamke (S. Mohamed, 2010), Harufu ya Mapera (K. Wamitila, 2012), Hujafa Hujaumbika (F. Kagwa, 2018), Haini (A. Shafi, 2002), na Ndoto ya Almasi (K. Walibora, 2006). Ngazi ya utambuzi ni mojawapo ya ngazi mbalimbali za ufokasi zilizopendekezwa na wananaratolojia. Kimsingi, ufokasi ni mtazamo ambao huchukuliwa katika kuwasilisha simulizi na kuikuza hadithi kwa ujumla. Data ya kuudhibiti na kuthibitisha madai ya mjadala wetu imetolewa katika riwaya teule. Uteuzi wa riwaya hizi unahalalishwa kwa misingi kwamba, hizi ni riwaya zilizo na matini pana zinazowezesha udondoaji wa mifano faafu inayodhihirisha ngazi za ufokasi na wakati huo huo kudhihirisha uamilifu wa ngazi hizo katika simulizi. Mjadala wa kimsingi katika makala haya umekitwa na kuongozwa na madai ya teneti za kimsingi za nadharia ya naratolojia ambayo inatambua ufokasi na uhusika kama vipengele muhimu katika uwasilishaji wa simulizi.