Main Article Content
Kufanana na Kutofautiana kwa Msamiati katika Lahaja za Lugha ya Kihaya: Mifano kutoka Kihamba na Kiziba
Abstract
Makala hii inafafanua dhana za kufanana na kutofautiana kwa msamiati wa lahaja ya Kihamba na Kiziba katika lugha ya Kihaya. Vipengele vinavyohusika katika kuchunguza kufanana na kutofautiana huko ni vipengele vya tahajia na matamshi. Lengo la ulinganishi na ulinganuzi huo ni kubainisha ikiwa kuna ufanano na utofauti wa kimsamiati unaojitokeza katika lahaja hizi mbili za lugha ya Kihaya yaani Kihamba na Kiziba. Kwa mujibu wa makala hii, eneo hili halijapewa aula na hivyo kumpa mtafiti laghba ya kulishughulikia. Data ya makala hii imekusanywa uwandani katika eneo la Kyamutwala inakozungumzwa lahaja ya Kihamba. Kwa upande wa Kyamutwala, mtafiti amekusanya data katika kata za Kamachumu, Ibuga, Muhutwe na Izigo. Katika eneo la Kiziba data imekusanywa kutoka kata za Buyango, Bugandika, Ruzinga na Bwanjai inakozungumzwa lahaja ya Kiziba. Data hii ya uwandani imepatikana kwa mbinu ya ushuhudiaji, hojaji, usaili na uchanganuzi wa matini za maktabani. Mtafiti alishuhudia namna mbalimbali za kitahajia/hijai na kimatamshi kuhusiana na msamiati wa Kihaya katika lahaja ya Kihamba na Kiziba. Aidha, data ilikusanywa kupitia hojaji ambapo watafitiwa 80 waligawiwa dodoso na kuzijaza kikamilifu. Kupitia mbinu ya usaili, mtafiti alifanya mahojiano ya ana kwa ana na watafitiwa wa makala hii na kuweza kubaini ulinganifu na usiganifu uliopo baina ya msamiati wa lahaja zinazoshughulikiwa katika makala hii. Data ya maktabani ilipatikana kwa mapitio ya matini mbalimbali zinazohusiana na mada inayoshughulikiwa katika makala hii. Utafiti huu umeongozwa na Nadharia ya Umuundo iliyoasisiwa na Ferdinand De Saussure. Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kwamba baadhi ya msamiati wa Kihamba na Kiziba hurandana na baadhi husigana. Pia zimetolewa sababau za kufanana na kutofautiana kwa msamiati wa lahaja hizo. Mtafiti wa makala hii anapendekeza tafiti fuatizi zifafanue kwa kina sababu za kutofautiana na kufanana kwa msamiati wa lahaja hizi tofauti na ilivyoelezewa katika makala hii kwani sababu ni nyingi. Aidha, makala hii itatoa hamasa kwa watafiti kufanya tafiti juu ya lahaja za lugha mbalimbali. Vilevile, makala hii inatoa mchango katika kukuza na kuendeleza lugha za Kibantu na taaluma ya isimu kwa ujumla. Pia itaongeza marejeleo faafu kwa watafiti wa isimu.