Main Article Content

Ulinganishi wa Msamiati baina ya Kikamba, Kigweno na Chasu: Tathmini ya Nadhariatete ya Ndugu na Ndugu wa Mbali


Fatuma Abadalah
Sarah Ndanu M. Ngesu
George Yesse Mrikaria

Abstract

Makala haya yanachunguza kiulinganishaji msamiati wa lugha tatu za Kibantu, mbili zinazungumzwa nchini Tanzania na lahaja mbili za Kikamba zinazozungumzwa nchini Kenya. Lengo la Makala haya ni kutathmini maoni ya Massamba (2017) kuhusu nadhariatete ya ndugu na ndugu wa mbali. Lugha zinazotambuliwa kuwa ‘ndugu’ ni zile zilizo katika mtagusano wa karibu na zile zinazojulikana kama ‘ndugu wa mbali’ ni lugha zinazotokana na fuko hilo moja lakini zilizo mbali kimasafa. Data iliyotumiwa katika makala haya ilikusanywa uwandani kupitia orodha ya msamiati wa msingi uliopewa wazungumzaji wa Kigweno, Kipare na lahaja mbili za Kikamba. Vilevile data hii imetajirishwa na uzoevu wa waandishi kama wazungumzaji wazawa wa lugha zinazojadiliwa. Katika kujaribu kuthibitisha “Udungu” wa lugha hizi tulitumia kigezo muhimu cha kiisimu cha Mbinu Linganishi ambayo hutumika kulinganisha lugha mbalimbali kwa lengo la kuonesha kama lugha hizo zinatoka katika fuko moja au zinatokana na mafuko ya lugha tofauti. Ingawa katika mbinu linganishi kuna mambo kadha yanayochunguzwa, tumejikita kuchunguza na kuchanganua msamiati wa msingi, mfumo wa maumbo ya maneno, maumbo ya sauti na mfumo wa uainishaji wa nomino katika lugha zinazohusika. Makala haya yamebaini kwamba kuna ulinganifu wa kiwango kikubwa, baina ya lugha za Kikamba, Kigweno na Chasu ingawa wazungumzaji wake wako katika nchi tofauti (Kikamba-Kenya, Kigweno na Chasu-Tanzania) na hawana utangamano wa kila siku. Kufanana huko kumebainika katika msamiati wa viunngo vya mwili kwa 52 %, msamiati wa mazingira asili kwa 59% na msamiati wa matendo ya kila siku kwa 65 %. Pia, imebainika kuna kutofautiana kwa msamiati wa viunngo vya mwili kwa 48 %, msamiati wa mazingira asili kwa 41 % na msamiati wa matendo ya kila siku kwa 35%. Msamiati mwingi unashabihiana kwa sauti na panapotokea tofauti ya sauti imebainika sauti hizo zinatamkiwa mahali pamoja au zimetokana na kuathiriwa na lugha jirani na pia kutokana utengano wa muda mrefu. Hivyo, lugha za Kikamba, Kigweno na Chasu zina mnasaba wa karibu jambo linalodhihirishwa na msamiati wa msingi pamoja na mfumo wa sauti. Aidha, wazungumzaji wa Kigweno na Chasu wanatangamana mara kwa mara nchini Tanzania na hivyo kama ilivyo Nadhariatete ya Ndugu na Ndugu wa Mbali kuna kufanana kwa msamiati kuliko lugha hizo zinavyofanana na Kikamba. Aidha, ilibainika kwamba kinyume na inavyodaiwa na Nadhariatete kwamba Ndugu wa Mbali watatofautiana kwa kiasi kikubwa, lahaja ya Kikamba ya Mwingi inayozungumzwa mbali sana, Kaskazini mwa Kaunti ya Kitui inashabihiana kisauti na lugha ya Chasu nchini Tanzania tofauti na lahaja ya Kikamba ya kimaandishi.


Journal Identifiers


eISSN: 2958-4914
 
empty cookie